Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema taifa linahitaji walimu bora na mahiri katika kufundisha pamoja na uwezo wa kukaa na kulea vizuri watoto wa Kitanzania ili wafikie malengo yao na kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali.
Waziri Mkenda ametoa rai hiyo mkoani Tanga wakati akifungua Mafunzo ya Kitaifa ya kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi wapatao 347, kutoka Wilaya za Korogwe Mji, Korogwe Vijijini na Lushoto kuhusu Uongozi, Usimamizi wa Shule na Utawala Bora yanayofanyika katika Chuo cha Ualimu Korogwe.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa mageuzi ya Elimu ndio agenda kubwa Duniani, na kwamba tayari Serikali ilishaanza kufanyia kazi mageuzi hayo ili kuendana na wakati pamoja na kukidhi mahitaji ya sasa na baadae ya Taifa na kitaifa.
“Hatutaki Ualimu uvamiwe, tunahitaji kuulinda pamoja na kuwasaidia Walimu kujiendeleza Kitaaluma. Hivyo kwenye Sera sasa hivi itakuwa ni lazima anayemaliza Chuo cha Ualimu aende akafanye mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja apimwe ili aweze kuhitimu kama kada zingine zinavyofanya” Alisema Waziri Mkenda.
Amesema azma ya Serikali ni kurudisha heshima ya Ualimu na kuhakikisha tunapata walimu wenye sifa stahiki, bora, wenye uwezo na umahiri wa kufundisha na kulea watoto kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Aidha amebainisha kwamba Serikali itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha Walimu wanathaminiwa katika kutenda kazi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali, kununua vifaa ikiwemo vishkwambi na kuweka mazingira rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa mpaka sasa Walimu wamefanya kazi kubwa, na kwamba bado kuna kazi kubwa zaidi inawahitaji kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
“Tunawaheshimu sana Walimu wote, na ni ukweli usiopingika Walimu ndio tegemeo letu kubwa sana hapa Nchini, mmechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika Elimu yetu, bila nyie hatuna elimu” Alieleza Mkenda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dk. Siston Masanja amesema mafunzo hayo yanatekelezwa kwa awamu ya pili, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST) kupitia afua namba 8 ambapo ADEM ilipewa jukumu na Wizara ya Elimu, kuendesha mafunzo kwa Walimu Wakuu 17,000 Nchini hasa kwa Tanzania Bara.
Amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilitekelezwa kati ya mwezi Septemba na Oktoba 2023 ambayo ilihusisha kati ya Walimu Wakuu 4,522 kutoka Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Njombe, Songwe, Morogoro, Dodoma na mkoa wa Mara.
“Awamu hii jumla ya Walimu Wakuu 4,620 kutoka Mikoa 6 ya Tanzania Bara watapatiwa mafunzo ikiwemo kutoka Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Kigoma, Mtwara, Simiyu na Mbeya. Zoezi hili litaendelea kwa Mikoa iliyobaki” alisema Dkt. Masanja.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema ameishukuru Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu ya Elimu kuanzia Elimu ya Awali mpaka Vyuo, na kwamba imeendelea kuchagiza maendeleo katika wilaya hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Mwenyekiti wa mafunzo hayo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kerenge Mlemwa iliyopo Korogwe Vijijini Philipo Chombo ameahidi watatumia vema ujuzi na maarifa watakayoyapa katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Wanafunzi na jamii kwa ujumla.