Katika hatua ya kukabiliana na magonjwa Yasiyoambukiza, Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa matembezi yaliyoandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) yanayojulikana kama ‘Walk the Talk, the health for all challenges’, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, alisema kuwa uzingatiaji wa mtindo bora wa maisha ukiwemo kufanya mazoezi na ulaji wa vyakula bora husaidia kupunguza hatari ya magonjwa Yasiyoambukiza kama vile Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu na Saratani.
“Katika juhudi za kutekeleza dira hii, Serikali imeanza kampeni ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ya mwili. Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, alizindua mpango wa kufunga barabara inayopitia Daraja la Tanzanite kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi,” alisema Waziri Mwalimu.
Akizungumzia umuhimu wa juhudi hizi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, alisema kuwa ni wakati muhimu sasa kwa jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya na kujikinga na magonjwa Yasiyoambukiza.
SomaZaidi;Mbinu Bora: Kuondokana na Unene Kupindukia kwa Afya Bora!
“Kwa sasa Duniani inaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la magonjwa Yasiyoambukiza, ambapo sababu kuu ni pamoja na kutofanya mazoezi, ulaji usio wa kiafya na matumizi yasiyo sahihi ya chumvi, sukari na mafuta,” alisema Dkt. Tedros.
Dkt. Tedros amewaomba nchi wanachama wa WHO kuhakikisha wanatolea jamii elimu sahihi kuhusu kujikinga na magonjwa haya pamoja na namna bora ya kutibu na kuishi na magonjwa hayo.
Juhudi hizi zinalenga kuimarisha afya ya wananchi na kupunguza athari za magonjwa Yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa ndio changamoto kubwa ya afya ya umma Duniani kwa miongo kadhaa iliyopita.