Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameanza ziara ya kikazi mkoani Mbeya ambapo anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya umeme mkoani hapa.
Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Dk. Biteko amepokelewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.
Katika kikao chake na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Biteko ameeleza jitihada zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu, Siasa na Nishati.
Katika Sekta ya Nishati, Dk. Biteko ameeleza kuwa, upungufu wa umeme nchini ni kati ya megawati 300 hadi 190 lakini kwa sasa kuna matumaini makubwa kwani mradi wa Julius Nyerere ( JNHPP) unatarajiwa kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa mwezi huu na matumaini mengine ni kutoka Mradi wa umeme wa Rusumo ambao utaingiza katika gridi megawati 27.
Amesema kuwa, kiasi hicho cha umeme kitakapoingia kwenye gridi ya Taifa kitaondoa hali ya sasa ya mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko uzalishaji na pia kuiwezesha Serikali kuendelea kufanya maboresho kwenye miundombinu ya umeme.
Amesema kuwa, kwa Mkoa wa Mbeya ambao mahitaji yake ni kati ya megawati 70 na 74 ambapo kwa sasa wanapata umeme wa megawati 51 na kueleza kuwa, jitihada zinazoendelea sasa zitapelekea Mkoa huo pia kupata umeme kulingana na mahitaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amepongeza Mkoa wa Mbeya kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na usimamizi mzuri wa sekta Elimu ambao watoto wanaostahili kwenda shule wameripoti kwa zaidi ya asilimia 70.
Dk. Biteko amesisitiza viongozi kufuata agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan la kuwa, tofauti ya itikadi ya vyama vya siasa isifanye wananchi kuwa maadui bali watu wabishane kwa hoja huku kipaumbele kikiwa ni maendeleo ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amemueleza Dk. Doto Biteko kuwa, shughuli za kiuchumi katika Mkoa huo zinaendelea vizuri na katika mwaka 2023/2024 walifanikiwa kukusanya mapato ya shilingi Bilioni 49 ikiwa ni zaidi ya asilimia 105.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi ya umeme inaendelea vizuri ikiwemo ya upelekaji umeme vijijini, vitongojini na migodini.
Katika elimu amesema kuwa, Mkoa huo umekuwa na ufaulu mzuri huku watoto wanaopaswa kwenda shule, wakiripoti kwa zaidi ya asilimia 70.