Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati matukio ya baadhi ya wananchi kupotea kwa madai ya kutekwa na watu wasiojulikana, kwani matukio hayo yasipothibitiwa yanaweza kusababisha machafuko siku za baadaye.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika jana Jumapili Juni 30, 2024 katika viwanja vya Handeni Square wilayani humo mkoani Tanga, Lema amesema wamepata taarifa kuhusu madai ya kupotea kwa mwanachama wao, Kombo Mbwana tangu Jumamosi, hivyo kuiomba Serikali ilifanyie kazi suala hilo.
Awali akielezea tukio la mwanachama wao kupotea, Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Kombo Matulu amekiri aliyepotea ni mwanachama wao na wamefuatilia sehemu mbalimbali na mpaka sasa hawajapata majibu mahali alipo.
Soma zaidi:CHADEMA Wazindua Ziara ya Kihistoria Kanda ya Kaskazini
Mama mzazi wa kijana huyo, Hellena Joseph, mkazi wa kijiji cha Komsala Handeni amesema tukio hilo lilitokea Jumamosi ya Juni 29, 2024, kwani alipokwenda nyumbani kwa mtoto wake asubuhi kumsalimia, alipewa taarifa na mkewe kuwa walifika watu nyumbani kwao na kumchukua kwa madai wanakaa kwenye eneo ambalo wamelinunua.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema tukio hilo lipo kwenye uchunguzi chini ya Jeshi la Polisi na wao kama Serikali bado halijawashinda wanalifanyiakazi, ili kijana anayedaiwa kutekwa apatikane na wafahamu nini kimemtokea.
Mwananchi imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi kwa njia ya simu kuhusu ufafanuzi wa madai ya taarifa ya kutekwa mwanachama huyo wa Chadema, ila simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyedai yupo kwenye kikao.