Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema Sekta ya utalii inaongoza kwa kuiletea nchi ya Tanzania fedha za kigeni ambapo sasa zimefikia dola za Marekani bilioni 3.37 (zaidi ya shilingi za Tanzania trilioni 8)
Amesema hayo wakati akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa habari Jumapili Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo amesema sekta ya utalii imemrejeshea shukurani Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki binafsi katika utengenezaji wa filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” inayotajwa kuchangia mafanikio hayo
Aidha Matinyi ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato ya dola za Marekani bilioni 1.31 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza dola bilioni 3.37.
Pia amesema kuwa idadi ya watalii iliongezeka baada ya mlipuko wa UVIKO-19 na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili Afrika kwa kutembelewa na watalii wengi baada ya Ethiopia, hivyo kuchochea zaidi mapato yaliyoifanya Tanzania kushika nafasi ya tatu baada ya Moroko na Morisi (Mauritius) kwenye ukusanyaji wa mapato yatokanayo na utalii.