Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia zimesaini mkataba wenye thamani ya Euro milioni 361.1 (sawa na takribani shilingi bilioni 988.093) kwa ajili ya kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam {Dar Es Salaam Metropolitan Development Project Phase II (DMDP II)}.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulunchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema DMDP II itaendelea kuboresha miundombinu muhimu ya umma katika Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni zilizokuwepo kwenye Awamu ya I ya mradi huo, sambamba na kupanua wigo wa uboreshaji miundombinu katika Wilaya zinazoingia katika mradi kwa mara ya kwanza za Ubungo na Kigamboni.
Alisema lengo la mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020 -2025 na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolenga kutanua na kuboresha miundombinu na huduma katika Jiji la Dar-es-Salaam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete alisema Benki hiyo inajivunia kuwa sehemu ya ukuaji wa Dar es Salaam ambapo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, benki hiyo imetenga dola bilioni 1.5 kwa ajili ya ufadhili maendeleo ya jiji hilo.
Alisema mfano mzuri wa matokeo ya ushiriki wao katika maendeleo ya Dar es Salaam unaonekana katika matokeo ya Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kuendeleza Miundombinu Dar es Salaam wa dola milioni 300 uliokamilika mwaka jana.
“Mradi huu ulijenga kilomita 207 za barabara na vituo vinne vya mabasi ambavyo vimeboresha usafiri kwa zaidi ya watu milioni 3.5 na kujenga kilomita 75 za mfumo wa maji na mabwawa matatu ya kuzuia mafuriko, kupunguza mafuriko kwa watu wanaoishi katika eneo la hekta 400 lenye hatari ya mafuriko”, alisema Bw. Belete.