Watendaji wa Halmashauri Mkoani Morogoro wametakiwa kuwa mahiri katika kuzuia hoja za Ukaguzi kutojitokeza katika Halmashauri zao badala ya kuwa mahiri katika kujibu hoja hizo wakati zimejitokeza na hivyo kuiletea doa Halmashauri wanazofanyia kazi.
Ushauri huo umetolewa Juni 21, 2024 na Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Morogoro Bw. Baraka Mfugale wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro.
Bwana Mfugale amesema, watumishi wengi wa Halmashauri wanakuwa mahiri katika kujibu hoja kuliko kuzuia ambapo amewataka kujitahidi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, Taratibu na Kanuni (STK) zilizopo hivyo kuto ruhusu hoja lakini pia kutoa ushirikiano wakati wa ukaguzi unapofanyika kwa lengo la kupata majibu sahihi kabla ya vikao kufanyika.
Soma :Mashina ya Migomba ni Utajiri Uliopindukia – RAS Morogoro
“Ni muhimu tukapata ushirikiano mzuri wakati wa ukaguzi kuliko ushirikiano mkubwa mnaouhitaji wakati wa kikao” amesisitiza Mfugale.
kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kwa lengo la kuendeleza Halmashauri hiyo, na kwa kufanya hivyo ni rahisi kuzuia hoja za ukaguzi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa maendeleo ya Wilaya hiyo watumishi wa Serikali wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuepusha migongano baina yao na kuwa malengo ya pamoja katika kufikia mafanikio ya maendeleo ya wananchi wa Malinyi.
“Team work ndani ya Halmashauri ya Wilaya Malinyi ni mbaya sana” Amebainisha Mhe. Adam Malima.
Aidha Mhe. Malima ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha matengenezo ya dharura ya barabara ya Malinyi, kuleta chakula kwa wananchi wa Malinyi walioathirika na mafuriko, lakini pia kwa kuto shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha Ifakara ambapo kitapunguza adha ya umeme Wilayani humo.