Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema hatua ya utatuzi wa hoja za Muungano imefikia pazuri hivyo ni jukumu la Serikali kuendelea kutoa elimu hususan kwa vijana ili wapate uelewa kuhusu Muungano.
Ameyasema hayo leo Juni 13, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohamed Haji aliyeuliza kuhusu umuhimu kwa Serikali kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu ya hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi hususan kwa vijana.
Akiendelea kujibu swali hilo, Waziri Mkuu amepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwani zimekuwa zikikutana kujadili hoja mbalimbali zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi hivyo kuufanya Muungano udumu.
“Ni kweli Tanzania ni matokeo ya Tanganyika na Zanzibar na Muungano huu ambao unatuunganisha wa Bara na Visiwani tunaendelea nao na tunayo mafanikio ya Muungano na mimi nikiwa ni sehemu ya vikao vya wajumbe wanaopitia hoja za Muungano naweza kusema hatua tuliyofikia sasa ni nzuri kwasababu hoja nyingi zimepatiwa ufumbuzi,” ameseme Waziri Mkuu.
Soma Zaidi:DK.Mwinyi Asisitiza Kudumisha Muungano
Amesema kuwa ni kweli vijana wengi wamezaliwa baada ya Muungano hivyo ni jukumu la Serikali kuendelea kutoa elimu hasa kupitia mitandao ya kijamii ili wajue faida zake.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa katika kikao cha Kamati ya Pamoja cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kilichopita, ilikubalika kuwa kila semina, makongamano au warsha zinapofanyika ajenda ya Muungano ni muhimu iwepo ili kufikisha kwa wananchi kueleza faida za Muungano na utatuzi wa hoja zake.
Hivyo, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Zanzibar wataendelea kuratibu yanayoibuka kulingana na mahitaji na kuyaorodhesha na kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ kuangalia namna ya kuzitatua hoja hizo.
“Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na Muungano imara, wenye maslahi kwa Watanzania wote lakini ambao pia utatusaidia kuendelea kutuunganisha Watanzania tuweze kuishi kama ndugu kama ambavyo tunaishi hivi sasa tumeendea kuwa wamoja,” amesisitiza Waziri Mkuu.