Wakati kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz Ki, akiandika waraka maalumu wa kuwashukuru wachezaji, viongozi, mashabiki na wafanyakazi wote wa timu hiyo kwa ushirikiano waliompa, klabu hiyo inatarajia kutangaza mikakati yake kuelekea msimu mpya kwenye mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika keshokutwa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Aziz Ki alifuta waraka huo uliongeza taharuki kwa mashabiki na wanachama wa Yanga muda mfupi baada ya kuuandika katika akaunti yake ya Instagram.
Soma Zaidi:Vita Ya Mfungaji Bora Ligi Kuu Yapamba Moto.
Aziz Ki ameendelea na sintofahamu kuhusiana na hatima yake baada ya kushindwa kutia saini mkataba mpya wa kuwatumikia mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabosi wa Yanga wamesema wanatarajia kujiimarisha kwa lengo la kupata mafanikio zaidi katika msimu mpya wa mashindano na hawakuwa tayari kuzungumzia andiko hilo la Aziz Ki, nyota raia wa Burkina Faso.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vyema na amewataka washiriki waliotajwa kwenye katiba yao ambao ni viongozi watano wa kila tawi kuhudhuria bila kukosa.
“Tuko katika maandalizi ya kuelekea mkutano wetu utakaofanyika Jumapili, huu ni Mkutano Mkuu wa Wanachama wa kikatiba, lakini hawahushiriki wote, wale viongozi ambao katiba inawatambua, ni viongozi watano kutoka kwenye kila tawi duniani kote ambako matawi ya Yanga wanapatikana.
Tunaamini viongozi wote wa matawi watakuja kwa wingi na utaongozwa na Rais Hersi Said, kila msimu ukimalizika ni lazima aje awaambie wanachama msimu ulivyokuwa na yale ambayo walimwagiza akayatekeleze kama kiongozi wao ameyatekeleza kwa asilimia ngapi, baada ya hapo kama wataafiki, tunakuja kupanga pamoja kuelekea msimu unaofuatia,” alisema Kamwe.
Aliongeza pamoja na mafanikio waliyopata msimu huu, Hersi atabainisha mikakati ambayo itaifanya klabu na timu yao kuwa imara zaidi na tishio Afrika katika msimu ujao wa mashindano.
Kuhusu Hafiz Konkoni, ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo katika timu ya Dogan Turk Birligi ya Cyprus, akitokea Yanga, alisema ni kweli anaidai fedha Yanga na wanajipanga kumalizana naye hivi karibuni.
“Ukiwa unaendesha soka kuna mambo yanajitokeza, kuna wachezaji wanakuja lakini wanashindwa kukupa kile unachotarajia, Hafiz ni kweli tulimwondoa kwenda klabu nyingine lakini tulipaswa tumlipe kiasi fulani cha fedha ili tumalizane naye, kuna kuchelewa kidogo katika malipo hayo.
Tutamlipa, uongozi wa Yanga siku za karibuni ulikuwa umelenga zaidi shughuli za kumaliza msimu, ajenda ya kumaliza madeni kwa wachezaji wote wanaotudai itafanyiwa kazi ndani ya siku tatu hizi ili twende dirisha la usajili kila kitu kikiwa kimekamilika,” Kamwe aliongeza.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limetangaza kuiondolea Yanga adhabu ya kufungiwa kusajili wachezaji baada ya kurekebisha upungufu uliojitokeza katika uhamisho wa mchezaji ambaye hakutajwa jina lake.
Yanga inatajwa haikuingiza uthibitisho wa malipo ya uhamisho wa mchezaji husika katika mfumo wa usajili (TMS), licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.
Hata hivyo shirikisho hilo limesema Yanga bado ina adhabu nyingine ya kufungiwa kusajili baada ya kushindwa kumalizana vyema na mchezaji wake, Lazarus Kambole, ambaye alifungua kesi ya madai ya malimbikizo ya mishahara na kuvunja mkataba bila ya kufuata taratibu.