Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imezindua rasmi utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, ambao una lengo la kuboresha huduma za afya katika ngazi ya msingi.
Mpango huo uliozinduliwa hapo awali mwezi Januari mwaka huu na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, sasa umeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Pwani. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, ametoa tangazo hilo leo wakati wa Semina Elekezi kwa Viongozi wa Mkoa huo na Wilaya zake.
Katika semina hiyo, Mhe. Kunenge alieleza kuwa Mkoa wa Pwani umepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango huo na kuahidi kuwa mkoa huo utakuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wake. Zoezi la kuchagua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii litafanyika kuanzia Halmashauri ya Kibaha Mji na Rufiji, ambapo jumla ya Wahudumu 480 wanatarajiwa kufikiwa.
SomaZaidi;Kuimarisha Afya Kupitia Mtindo Bora Wa Maisha
Mganga Mkuu wa Mkoa huo aliyezungumza katika semina hiyo amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ili kuhakikisha malengo yanafikiwa. Aidha, mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dkt. Meshack Chinyuli, alieleza kuwa mpango huo unalenga kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii ili kufikia lengo la afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.
Serikali imedhamiria kufikia jumla ya Wahudumu 137,294 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara katika kipindi cha miaka mitano. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii na kufikia dhana ya afya kwa wote.
Mpango huu unalenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya, na kujenga jamii yenye afya bora na ustawi wa kijamii.