Msanii maarufu wa Nigeria, Habeeb Okikiola, anayejulikana kwa jina la kisanii Portable, ameibua masikitiko makubwa na shutuma kali dhidi ya mwenzake, Davido.
Portable amedai kuwa Davido alimpa ushauri mbaya ambao unaonekana kudhoofisha malengo yake ya kusaini mkataba na lebo ya muziki inayoweza kumsaidia kufikia mafanikio makubwa zaidi katika tasnia hiyo.
Katika kikao cha moja kwa moja kwenye Instagram, Portable alifichua kuwa Davido alimshauri asisaini na Sony Music, lebo ambayo Davido mwenyewe amesaini nayo, na badala yake akamshauri kusaini na lebo ya Empire. Portable alisema, “Unasaini na Sony Music, lakini unanipa ushauri mbaya Marekani kusaini na Empire na kuchukua malipo ya awali. Grammy unayoifukuzia ndiyo ninayoifukuzia pia”
Msanii huyo alieleza kuwa anahisi ushauri huo hauna nia njema na kwamba unalenga kumrudisha nyuma katika jitihada zake za kufikia tuzo za Grammy kama Davido.
Mbali na ushauri huo, Portable amefunguka zaidi juu ya hisia zake, akimshutumu Davido kwa kumtumia tu kwa ajili ya kutafuta umaarufu bila kumpa msaada wowote wa maana. Alisema, “Davido alinitumia kwa ajili ya kutrend. Hukunipa pesa wala verse yoyote, na kisha ukanipost huyo ni Superstar.” Haya yalikuwa ni maneno mazito ambayo yameibua mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhusiano kati ya wasanii hawa wawili.
SomaZaidi;Davido vs. Wizkid: Mizozo Yawasha Moto Mtandaoni
Kilio cha Portable kinaonekana kuwa na uzito zaidi alipodai kuwa alilazimika kutumia daraja la kwanza (First Class) kusafiri kwenda Marekani ili kukutana na Davido, jambo ambalo limeongeza machungu yake kwa kile anachodai kuwa ni kutothaminiwa na msanii huyo mkubwa
Katika hatua za hivi karibuni, Davido amem-unfollow Portable kwenye Instagram, hatua ambayo imezidi kuongeza ukakasi kati yao. Ugomvi wao wa hadharani unazidi kufuatiliwa kwa karibu na mashabiki wao pamoja na vyombo vya habari, huku kila mmoja akitoa maoni yake kuhusu nani ana makosa katika mzozo huu.
Portable pia aliongeza kuwa anatamani msaada kutoka kwa watu ambao wanamsaidia kwa dhati bila kumsikiliza maneno ya uzushi au kumpa ushauri mbaya. Alimpongeza Olamide na Skepta kwa msaada wao wa moja kwa moja, akisema, “Olamide alinisaidia moja kwa moja, Skepta alinipe verse, pesa, viatu, nguo, na kunifanya nijuane na brendi kubwa za mitindo. Huo ndio msaada ninaotaka kutoka kwa Mungu, siyo mtu anayefuatilia maneno ya uzushi”
Kufuatia shutuma hizi, wadau wa muziki na mashabiki wanashangaa ikiwa kutakuwa na majibu yoyote kutoka kwa Davido au kama ugomvi huu utaathiri vibaya mahusiano ya kikazi na ya kibinafsi ya wasanii hawa. Ni wazi kuwa mzozo huu unaangazia changamoto na ushindani unaowakabili wasanii katika tasnia ya muziki, hususan katika juhudi zao za kufikia mafanikio na kutambuliwa kimataifa.