Wakazi wa eneo la kibiashara Kariakoo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutoweza kuzingatia muda sahihi wa kula chakula, na hali hii inaleta matatizo ya kiafya miongoni mwa wafanyabiashara.
Wengi wao wanakiri kukosa muda wa kupumzika na kula vizuri kutokana na shinikizo la kufanya kazi na kupambana na umasikini.
Juma Onary, mfanyabiashara wa eneo hilo, alielezea jinsi hali ngumu ya maisha inavyowafanya washindwe kupata mlo kamili kwa wakati unaofaa. Umasikini uliokithiri unaathiri uwezo wao wa kumudu muda wa kula chakula kwa utulivu na kufuata viwango sahihi vya lishe. “Tunahangaika kuendesha biashara zetu na mara nyingi tunakosa muda wa kupumzika na kula vizuri,” alisema Omary.
Read More: Food Vendors Add Yeast to Ugali to Increase Sales
Athari za kutotii muda sahihi wa kula chakula zinajitokeza kwa mfanyabiashara wa bodaboda Lucas Alexander ambaye alisema kuwa harakati zake za kila siku zimemfanya kukosa muda wa kula chakula cha kutosha. Hali hii imepelekea matatizo ya kiafya kwake, ikiwa ni pamoja na vidonda vya tumbo. Hii ni changamoto kubwa kwa watu wengi ambao wanahitaji kufanya kazi kwa bidii na hawana muda wa kula vyakula vyenye lishe bora.
Mbali na hilo, Mwajuma Hamza, mfanyabiashara mwingine wa eneo hilo, alielezea wasiwasi wake juu ya ubora duni wa vyakula vinavyopatikana Kariakoo. Alisema kwamba vyakula vingi havifuati viwango vya usafi na hii inaweka afya za watumiaji hatarini. Kutokana na hali hiyo, watu wengi wameamua kukaa njaa wakati wa kazi na badala yake kunywa maji ili kuhifadhi afya zao.
Changamoto ya kutotilia maanani muda sahihi wa kula chakula inaonekana kuwa tatizo kubwa kwa wananchi wa Kariakoo. Hali ngumu ya maisha na umasikini vimekuwa vikisababisha watu kukosa mlo kamili na kuathiri afya zao. Aidha, ubora duni wa vyakula vinavyopatikana katika eneo hilo umesababisha watu kuepuka kula ili kujikinga na madhara ya kiafya. Ni wakati sasa kwa wadau husika kushirikiana na kutafuta suluhisho la changamoto hii ili kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora na wanazingatia muda sahihi wa kula chakula kwa ajili ya afya yao na ustawi wa jumla