Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi,(CCM) Dk Emmanuel Nchimbi amehitimisha ziara yake ya mikoa 11,huku akitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa,wilaya na wakurugenzi kuhusu usimamizi wa fedha za miradi zilizopelekwa kwenye maeneo yao.
Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Tanga wakati akihitimisha ziara yake iliyofanyika katika mikoa 11 ,katika uwanja wa Lamore, amesema Serikali imetoa fedha nyingi za miradi katika maeneo mbalimbali, hivyo viongozi wote husika lazima wasimamie miradi hiyo.
Amesema fedha hizo lazima zikafanye kazi iliyokusudiwa kwa kuwaambia watumishi wao, kwamba ni kosa kubwa kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa shughuli zao nyingine.
Soma:Nchimbi Akoshwa Ubunifu Wa Wanachuo Wa KM Nyerere
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mohamed Salim Ratco amesema wapo baadhi ya watumishi katika halmashauri za Mkoa wa Tanga wanafanya ubadhilifu wa fedha za miradi inayofanyika kwenye maeneo yao, hivyo kuomba wachukuliwe hatua na yupo kwenye utaratibu wa kuwataja watumishi hao.
Ameiomba Serikali kuangalia utaratibu wa watumishi wote ambao wanafanya ubadhirifu wasihamishe,ila wachukuliwe hatua na kuondolewa kwenye nafasi zao za kazi, kupisha uchunguzi au kuchukuliwa hatua kutokana na ubadhirifu wa fedha waliofanya.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwao,kwani wamebaini utekelezaji wa ilani ya uchaguzi umefanyika kwa miradi mingi kufanyika kwenye mikoa na wilaya ambazo wamepita.