Rais wa Rwanda Paul Kagame amekubali kukutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi kujadili mzozo unaoendelea Mashariki mwa Congo.
Makubaliano hayo yalifuatia mkutano wa Jumatatu katika mji mkuu wa Angola Luanda kati ya Kagame na Rais wa Angola João Lourenço, mpatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro wa DR Congo.
“Iliamuliwa kuwa Rais Kagame atakubali kukutana na Rais Tshisekedi katika tarehe itakayowekwa na mpatanishi,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Tete Antonio aliambia wanahabari baada ya mkutano huo.
Antonio amesema kuwa Rwanda na DR Congo zimekubali kufanya mkutano huo, huku wajumbe wa mawaziri kutoka pande zote mbili wakishughulikia mpango huo.
Ofisi ya rais wa Rwanda ilisema kwenye mtandao wa X kwamba viongozi hao wawili “walikubaliana juu ya hatua muhimu za kushughulikia sababu kuu za mzozo”.
DR Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23, tuhuma ambayo Kigali imekanusha.
Source: BBC