Leo, tarehe 04 Mei 2024, saa 12:00 Asubuhi – Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa tahadhari kali kwa wananchi wakati kimbunga “HIDAYA” kinavyosogea karibu na pwani ya Tanzania. Kimbunga hicho, chenye mgandamizo wa hewa wa 985 hPa na kasi ya upepo inayofikia kilomita 120 kwa saa, kinatishia kuleta madhara makubwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, na Dar es Salaam, pamoja na visiwa vya Zanzibar.
Soma Zaidi;Kimbunga “HIDAYA” Chakaribia Pwani ya Mtwara
Hadi saa 9 usiku wa kuamkia leo, kimbunga “HIDAYA” kilikuwa kwenye eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia, na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es Salaam. Athari za kimbunga hicho zimeshuhudiwa tayari, huku vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vikiripotiwa katika maeneo hayo. Vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, na Dar es Salaam vimeripoti upepo mkali unaovuka kilomita 50 kwa saa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.
Mikoa ya Mtwara na Lindi imeathiriwa zaidi na mvua kubwa, huku kituo cha Mtwara kikiripoti jumla ya milimita 75.5 za mvua ndani ya masaa 12 tu. Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ikilinganishwa na wastani wa mvua kwa mwezi Mei katika kituo cha Mtwara ambacho ni milimita 54 tu. Hivyo, kiwango cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 12 katika kituo cha Mtwara kinakadiriwa kuwa asilimia 140 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei.
Soma Zaidi;Cyclone “HIDAYA” Threatens Tanzanian Coast
TMA inatabiri kwamba kimbunga “HIDAYA” kitaendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya Tanzania, huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili, tarehe 05 Mei 2024. Katika kipindi hiki, kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kusababisha mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani, hasa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, na Dar es Salaam, pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani. Matukio ya mawimbi makubwa baharini pia yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa Bahari ya Hindi.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wote wanaoishi katika maeneo yaliyotajwa na wale wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari. Ni muhimu kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na kufuata maelekezo ya mamlaka husika. Tahadhari zaidi inapaswa kuchukuliwa katika maeneo ya pwani, ikiwa ni pamoja na kuepuka kwenda baharini na kuzingatia usalama wa maisha na mali.
Hali hii inahimiza umuhimu wa kuwa na utayari wa hali ya hewa mbaya na kuzingatia usalama kwa kila mmoja. TMA inaendelea kutoa taarifa za hali ya hewa ili kuhakikisha usalama na ustawi wa wananchi wote.