Watu 16 familia moja waleweshwa na kuibiwa na Mganga wa jadi
Mkuu wa Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro amesema wanafanyia uchunguzi tukio la Mtu mmoja aliyejifanya Mganga wa jadi maeneo ya Mji mwema, Kigamboni aliyewanywesha na kuwalewesha dawa inayodhaniwa kuwa ni sumu Watu 16 wa Familia moja kisha kuwaibia simu.
“Tukio hilo limetokea February 18, 2024 majira ya saa tatu usiku wakati Mtu huyo alipofika nyumbani kwa Familia ya Mzee Halisi Amani kwa lengo la kumtibu Mke wake Fatuma Abdalla (52) aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo la miguu ambapo aliwanywesha dawa iliyowalewesha Familia nzima, wakapoteza fahamu na akawaibia simu 5 za mkononi na kuondoka nazo” – Kamanda Muliro.
“Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamtafuta Mganga huyo lakini limemkamata kwa mahojiano Mtu mmoja aitwae Jalala Ally Said anayedaiwa kushirikiana na Mganga huyo lakini kwa upande wa Wagojwa walilazwa na kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni na hadi sasa 13 kati yao wamesharuhusiwa huku watatu wakiendelea kupata matibabu na hali zao zinaendelea vizuri” – Kamanda Muliro.
“Tukio lingine limetokea tarehe 9 Februari, 2024 huko eneo la Tuangoma, Mbagala ambapo Mtu mmoja aliyejifanya Mganga wa jadi aliwanywesha Watu watano dawa zilizowalevya na baadae kupoteza fahamu na kuwaibia pikipiki namba MC474, simu 3 za mkononi na Tsh 30,000, Jeshi la Polisi linawatahadharisha Wananchi kuhusiana na uwepo kwa Watu wanaojifanya waganga wa jadi ambao huwalewesha Watu na wanafamilia kwa ujumla na baadae kuwaibia” – Kamanda Muliro.