Serikali imesema ilifuta leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalibainika kufanya makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uhamishaji wa fedha kwenda nje ya nchi bila idhini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hayo yalielezwa katika kikao cha bunge kilichofanyika Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipojibu swali kutoka kwa Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kufahamu sababu za kufungwa kwa maduka ya kubadilisha fedha na athari ya upoteaji wa ajira kwa wananchi.
Mhe. Chande alieleza kuwa mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua kuwa baadhi ya maduka yalikuwa yakifanya miamala kinyume cha sheria na kanuni zinazosimamia shughuli za maduka ya fedha za kigeni na kudhibiti utakasaji wa fedha haramu.
“Katika miaka ya 2018 na 2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operesheni maalum ya ukaguzi katika maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali ambayo yalisababisha Serikali kufuta leseni kwa wale waliokiuka sheria kulingana na Kanuni ya 36 (1)(b) na 2 (d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 iliyorekebishwa mwaka 2019,” alisema Mhe. Chande.
Read>> http://KANUNI Bank of Tanzania https://www.bot.go.tz › Publications › Regulations
Aidha, Mhe. Chande alifafanua kuwa makosa mengine yaliyobainika ni pamoja na kutowatambua wateja kabla ya kutoa huduma kulingana na Sheria ya Udhibiti wa Utakasaji Fedha Haramu, Sura 423, na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakasaji Fedha Haramu.
Pia, aliongeza kuwa kosa lingine lilikuwa ni kugawa miamala ya wateja ili kuepuka kuweka rekodi muhimu zinazothibitisha uhalali wa miamala, kinyume na Kanuni ya 23 ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015, na kutowapa wateja stakabadhi za miamala kulingana na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni hizo.
Mhe. Chande alibainisha makosa mengine ambayo ni pamoja na kutowasilisha taarifa sahihi za miamala kwa Benki Kuu na hivyo kuhatarisha upatikanaji wa takwimu muhimu kwa shughuli za kiuchumi. Baadhi ya maduka pia yalibainika kuhusika katika uhamishaji wa fedha kwenda nje ya nchi bila idhini.
I am not real superb with English but I get hold this rattling leisurely to interpret.