Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikihitimisha jana awamu ya kwanza ya maandamano yake katika mikoa 13 nchini, Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, ametoa tathmini ya maandamano hayo kwamba yalilenga mambo manne.
Miongoni mwa mambo hayo ni kueleza Watanzania namna Tume Huru ya Uchaguzi iliyoundwa kisheria hivi karibuni ilivyo na matobo.
Akihutubia mamia ya wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika Uwanja wa Mashujaa, mjini hapa, Mbowe amesema mfumo wa uchaguzi kama ulivyo sasa nchini una matobo na unatoa upendeleo wa makusudi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda bila ridhaa ya wananchi.
Soma Zaidi:Chadema Members Demonstrate in Mbeya for Reforms in Gov’t.
“Maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa ambayo tunahitimisha leo (jana) Moshi, yalikuwa na malengo manne ambayo ni kushinikiza kupata katiba mpya na katiba bora itakayotibu maumivu, uonevu, utawanyaji wa rasilimali za nchi na itakayoleta utawala bora na kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
“Tuliamini tunapaswa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo itasababisha kupatikana kwa viongozi wenye hofu ya Mungu wanaopatikana katika chaguzi huru na chaguzi za haki. Lakini mfumo wetu wa uchaguzi kama ulivyo leo, ni mfumo wenye matobo ambao unatoa upendeleo wa makusudi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda bila ridhaa ya wananchi,“ alisema huku akibainisha katika mikoa hiyo ametembea kilomita 111.
“Tumeanza maandamano Aprili 22 nimetembea kilomita za kutosha. Tunapohitimisha hapa (Moshi) Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, yuko Morogoro anahitimisha. Tunaanza tena awamu ya pili katika mikoa yote iliyobakia na kama hawasikii tukimaliza tunaanza kwenye wilaya,” ameongeza.
Mpaka sasa awamu ya kwanza ya maandamano ya ngazi ya mikoa, CHADEMA imefanya katika mikoa ya Kagera, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Simiyu, Dodoma, Morogoro, Singida, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Benson Kigaila, ametaja chanzo cha matatizo yote hayo ni ya ugumu wa maisha, ni utawala wa CCM na kuwataka kuunganisha nguvu pamoja na kuleta mabadiliko.
“Maisha ni magumu, vitu vimepanda bei mwananchi wa hali ya chini anateseka, hii yote ni kutokana na kukosekana kwa utawala bora wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).Tujiunge na CHADEMA tuiuwe CCM katika chaguzi za serikali za mitaa mwaka 2024 na matanga yao yawe 2025 katika serikali kuu,” amesema Kigaila.
Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Jafary Michael, amewataka wananchi kujitokeza kujitetea katika kujiletea maendeleo na kuleta mabadiliko chanya kwa taifa.
Aidha, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Grace Kiwelu, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika chaguzi za serikali za mitaa ili kuondoa mapandikizi ya CCM yaliyowekwa na hayati John Pombe Magufuli.
“Tukimaliza uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 twendeni kwenye uchaguzi mkuu 2025 na kuhakikisha tunaleta mabadiliko na kukomboa majimbo yote yaliyochukuliwa CCM,” amesema Kiwelu.
Awali, Mwenyekiti wa CHADEMA Moshi Mjini, Raymond Mboya, amesema tangu Manispaa ya Moshi kuchukuliwa na CCM, masoko yameungua zaidi ya mara tatu.
“Wananchi wamepoteza mikopo na serikali ilitoa mwezi mmoja ili kujenga soko, lakini hadi sasa miezi mitatu soko hilo halijajengwa, zipo taarifa kuwa wapo vigogo wa manispaa ya Moshi wanashindana ili kupata tenda na hii ndiyo inayochelewesha ujengaji wa soko hilo.
Kuna ujenzi wa stendi ya Ngangamfumuni tulipokuwa madarakani, tulijenga ghorofa mbili lakini hadi sasa hapajaendelezwa hata kidogo kwa takribani miaka mnne hii inaonyesha jinsi gani CCM hawana mpango na maisha ya wananchi katika kuwaletea mabadiliko na maendeleo,” amesema Mbowe.