Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata dereva wa basi la kampuni ya Shabiby, Sadick Marugul, akituhumiwa kusababisha ajali iliyojeruhi watu 22 mapema leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP. Alex Mkama, amesema ajali hiyo imetokea katika eneo la Kihonda kwa Chambo, karibu na daraja la mwendokasi, baada ya dereva huyo kulazimisha kuyapita magari mengine katika eneo ambalo haliruhusiwi kisheria.
“Ni aibu kubwa kwamba dereva huyu ameamua kuyapita magari mengine katika eneo ambalo haliruhusiwi. Hii imesababisha ajali mbaya ambayo imejeruhi watu wengi,” alisema Kamanda Mkama.
Daktari wa magonjwa ya dharura wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dkt. Nafsa Marombwa, amesema majeruhi watano kati ya wale 22 waliobaki wana hali ngumu na wanaendelea kupatiwa matibabu ya dharura.
“Tumekabidhiwa jumla ya wagonjwa 22 ambao wamejeruhiwa katika ajali hii. Kati yao, wagonjwa watano wana hali ngumu na tunaendelea kuwapa matibabu wa dharura,” alisema Dkt. Marombwa.
SomaZaidi;Lori la Mafuta Lapata Ajali Sekenke
Kamanda Mkama amesema kuwa polisi wanafanya uchunguzi kina ili kubaini sababu halisi za ajali hiyo na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya dereva huyo.
“Tunatoa pole kwa Abiria na majeruhi wote katika ajali hii. Polisi wanafanya uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya dereva huyu,” alisema Kamanda Mkama.
Ajali hii imetokea siku ambayo Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, kufanya maadhimisho ya miaka 20 ya baraza hilo jijini Dar Es Salaam. Ajali hii inaonyesha kuwa jitihada za kukuza usalama barabarani bado zinahitaji kuimarishwa zaidi nchini.