Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omari ametoa wito kwa Waislam wote nchini kuendelea kutenda matendo yaliyomema hata wakiwa nje ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Sheikh Wald ameyasema hayo leo, katika Msikiti wa Kichangani uliopo Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo amewataka Waislam wote kujifunza maisha waliyonayo ndani ya Mwezi wa Ramadhani na waishi hivyo hivyo siku zote.
“Katika Mwezi wa Ramadhani Waislam wote wanatakiwa wamuoneshe asiyekuwa Muislam kwamba, uonekane ukarimu wake, huruma na huzuni yake, mpaka aiyekuwa Muislam atamani kuwa Muislam ’’alisema Sheikh Walid.
Alisisitiza pia kuwa dini ya Kiislam sio dini ya dini ya kigaidi wala ya kuua Watu bali dini hiyo ni dini ya amani na kutenda mema kwa watu wote hata wasiyokuwa Waislam.
“Si ajabu kuwa utasikia watu huko wakisema kuwa Uislam ni dini ya kigaidi kazi yake ni kuuwa Watu la, Uislam siyo dini ya kigaidi kwani ninavyowaona Waislam ndani ya Mwezi wa Ramadhani ndivyo walivyo’’ alifafanua Sheikh Walid.
Pamoja na hayo, ameongeza kuwa wanavyuoni waliopita wote walisema kuwa Mwezi wa Ramadhani ni Mwezi wa kimapinduzi na ni Mwezi wa kuwageuza watu fikra na kuwarudisha watu wote katika Uislam.