Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko makubwa kutokana na kifo cha kusikitisha cha mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath.
Mnamo tarehe 17 Juni 2024, mwili wa Asimwe, mwenye umri wa miaka miwili na nusu, ulipatikana ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi huku baadhi ya viungo vyake vikiwa havipo
Asimwe, mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilaya ya Muleba mkoani Kagera, alitekwa nyara mnamo Mei 30, 2024. Mama yake, Judith Richard, alieleza kuwa watekaji walijifanya wanahitaji msaada wa haraka baada ya kuumwa na nyoka. Walipofungua mlango kuwasaidia, walimnyonga na kumchukua mtoto wake
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel, alithibitisha kuwa watu watatu, akiwemo baba wa mtoto huyo, wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hili. Aliendelea kusema kuwa juhudi za kumsaka mtoto huyo zilikuwa zinaendelea kwa nguvu zote
SomaZaidi;Polisi Afrika Mashariki Waungana Waadhimisha Mauaji Ya Kimbari
Tukio hili limevutia hisia kali kutoka kwa mashirika mbalimbali, ikiwemo Tanzania Albino Society (TAS). Mwenyekiti wa TAS, Godson Mollel, alilaani vikali tukio hili na kusema kuwa ni aibu kwa taifa linalojigamba kuheshimu utu wa binadamu kuwa na raia wake wenye ualbino wakiishi kwa hofu. Alisisitiza umuhimu wa serikali kuchukua hatua kali na za haraka kukomesha vitendo vya kinyama kama hivi
Dr. Abel Nyamahanga, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, ameelekeza viongozi wa vijiji kufanya sensa ili kubaini na kulinda watu wenye ualbino katika wilaya hiyo. Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuhakikisha kuwa wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria
Kwa muda mrefu, watu wenye ualbino wamekuwa wakikabiliwa na manyanyaso na mauaji kutokana na imani potofu za kishirikina. Tukio hili linaonyesha kuwa tatizo hili bado lipo, licha ya juhudi za serikali na mashirika mbalimbali za kupambana na unyanyasaji huu.
Wakati jitihada za kuwasaka wahusika zikiendelea, wananchi na viongozi wanatoa wito kwa serikali kuongeza juhudi za kulinda maisha ya watu wenye ualbino na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa waathirika wa vitendo vya kikatili kama hivi.