Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden, Mhe. Diana Janse, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimueleza kuhusu nchi yake kuandaa Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaolenga kuongeza ushirikiano katika Nyanja za kiuchumi na kibiashara.
Aidha Mhe. Diana Janse, alisema kuwa nchi yake inatambua kuwa mradi wa Reli ya Kisasa ni moja ya miradi ya kipaumbele kwa Tanzania na kwamba nchi yake iko tayari kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.
Pia Janse amesema kwamba mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Sweden utajielekeza zaidi katika masuala ya kiuchumi na kibiashara ambapo utalenga zaidi kuvutia uwekezaji kupitia sekta binafsi.
Hata hivyo, Mhe. Dkt. Nchemba aliishukuru Sweden kwa kusaidia maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika sekta za nishati, elimu, maendeleo ya Jamii kupitia Mfuko wa TASAF pamoja na mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa SGR, kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida ambacho ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 96.
Pamoja na hilo, Dkt. Nchemba ameishukuru Sweden kwa kuonesha nia ya kutoa zaidi ya dola za Marekani milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha reli ya kisasa SGR, fedha ambazo nchi hiyo itazitoa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa tathimini ya mazingira ya mradi huo.
Kuhusu Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Nchemba aliahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika kufanikisha mkakati huo na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Sweden kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini ili kuchochea akuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Alisema Aidha, katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Balozi wa Sweden Nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias na naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, Viongozi hao walijadili kuhusu uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam ambapo nchi hiyo inataka kuwekeza kupitia kampuni ya Scania, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya usafiri katika jiji hilo la kibiashara.