Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kuingia uwanjani na kutoa taulo katika mchezo dhidi ya Mashujaa FC.
Taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetaja sababu za faini hiyo kwa simba.
“Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wakepamoja na walinzi wake wa uwanjani (stewards) kupanga njama na kufanikisha azma ya kuingia uwanjani na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina wakati mchezo tajwa hapo juu ukiendelea kwenye uwanja wa Azam Complex Machi 15, 2024”.
Mashabiki hao walionekana kupitia video fupi iliyosambaa mitandaoni wakijadiliana na mlinzi wa uwanjani (steward) kabla hawajaingia uwanjani kufanya tukio hilo lililoleta taswira mbaya kwa Ligi yetu.
Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Walinzi wa uwanjani (stewards) wa klabu ya Simba, Kessy Mohamed, Mrisho Mindu Pamoja na Mohamed Salmin pamoja na shabiki aliyefahamika kwa jina la Mohamed Saleh, wamefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 (kumi na miwili) kwa kosa la kushiriki katika tukio la mashabiki kuingia uwanjani wakati mchezo tajwa hapo juu ukiendelea.
Bodi inaendelea na uchunguzi wenye lengo la kufahamu wahusika wengine wa tukio hilo ambao hawakutambulika mara moja ili wachukuliwe hatua kali za kikanuni.
Adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Simba inawajibika kuhakikisha mashabiki na viongozi walioadhibiwa wanatii adhabu zao na kuzitekeleza kikamilifu ili kuepuka
klabu kuadhibiwa zaidi kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 47:5 ya
Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inalaani vikali vitendo vinavyoashiria imani za
kishirikina vinavyofanywa na wachezaji, mashabiki na maafisa wa klabu
kwani vitendo hivyo vimekuwa vikichafua taswira nzuri ya Ligi pamoja
na kushusha hadhi ya Ligi yenyewe.
Bodi imepanga kuchukua hatua kali zaidi za kikanuni kwa yeyote
atakayebainika kushiriki vitendo hivyo kuanzia tarehe ya taarifa hii na
Afisa Usalama wa Klabu husika atawajibika kwa asilimia 100 kisha
kuchukuliwa hatua kali kwa tukio lolote la aina hii litakalotokea.