Serikali imeiagiza Bodi ya Maziwa Nchini kujadili kwa haraka na kutatua tatizo la vifungashio vya maziwa vinavyofanya bei ya maziwa kuwa juu na kufanya wananchi kushindwa kumudu bei hivyo kuongeza hali ya udumavu kwa watoto nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti wakati akifunga maadhimisho ya 27 ya wiki ya maziwa duniani, yaliyofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, na kusema bei ya maziwa ipo juu na alipouliza sababu ikawa ni bei ya vifungashio hivyo bodi ione namna ya kutumia rasilimali za mbao kutengeneza vifungashio badala ya nailoni zinazotumika sasa ili kupunguza bei ya maziwa.
Mnyeti alisema bei ya maziwa ikishuka mtoto wa kitanzania atafanikiwa kunywa walau lita moja kwa wiki na kuwa suluhisho tosha la udumavu katika taifa ambalo kwa sasa bado lipo maeneo mbalimbali.
“Tuna tatizo kubwa sana katika taifa letu, tatizo kubwa la udumavu, na tatizo hili linatokana na watoto kutopata virutubisho bora ambavyo vinapaswa kupatikana katika miili yao, na udumavu unapokomaa mtoto anakosa akili, mtoto asipopata virutubisho vinavyotakiwa tunatengeneza taifa la watoto wasiokuwa na akili na tafsiri yake ni kwamba baadae hatutakuwa na maprofesa, madokta, kwa sababu watoto tunaowalea leo hawana virutubisho vinavyotakiwa” alisema Mnyeti.
Aliongeza kuwa maziwa yanaonekana kama kinywaji cha anasa, kwamba anayekunywa maziwa ni anayefanya starehe, na kwa watanzania hatuna utamaduni wa kunywa maziwa kwa sababu tunaona kunywa maziwa ni starehe jambo ambalo linafanya kuwa kizazi kisicho kuwa na uelewa.
Aliweka bayana kuwa serikali inagawa mbegu bora za ng’ombe na ameitaka chama cha wafugaji kuwahamasisha wafugaji kwenda kwenye vituo kuchukua madume kwa ajili ya kupanda ili ng’ombe atakayezaliwa awe ng’ombe mwenye ubora atakayetoa maziwa ya kutosha, na maadhimisho haya mwakani yafike mikoa ambayo wana udumavu mkubwa ili elimu itolewe kwa wananchi.
Mwenyekiti wa bodi ya washauri wa bodi ya maziwa Profesa Zakaria Masanyiwa, alisema katika siku 5 ambazo maadhimisho hayo yalifanyika wadau mbalimbali wamepata fursa ya kujifunza, kupata elimu na ujuzi na kupata maarifa mbalimbali yanayohusiana na tasnia nzima ya maziwa na kutoa wito kwa wananchi na watanzania wote kutumia elimu, ujuzi na maarifa hayo kwa ajili ya maendeleo ya tasnia ya maziwa.
Msajili wa bodi ya maziwa Profesa George Msalya alisema zaidi ya watu 5000 walitembelea mabanda katika maonesho hayo na kutoa elimu kwa wajasiriamali watakaokwenda kuitumia elimu waliyoipata kuongeza thamani ya maziwa ili kuona faida ya maziwa.
“Tumetoa elimu shuleni kwa wanafunzi, tumewatembelea watoto wenye mahitaji maalum, ttmewatembelea wagonjwa hospitalini, na bado jitihada zinaendelea” alisema Msalya
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Profesa Daniel Mushi alisema wameshaanza kuzishughulikia changamoto zinazoikabili tasnia ya maziwa ili iweze kuwa na tija kwenye uchumi wa kaya na taifa ikiwemo kuhamasisha vijana katika uzalishaji wa maziwa na kukabiliana na uholela wa bei za maziwa nchini.