WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia iliyoanza kusambaa inayofanywa na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya kubana fedha za miradi na kuzitumia kinyume na mipango.
“Jana nilikuwa Bunda na leo hapa Butiama nimekuta huu mchezo ambapo Halmashauri yenu inatumika kama kichaka. Wachache wenye mamlaka humu ndani wanatumia mwanya wa mwisho wa mwaka wa fedha na kuhamisha fedha zilizoletwa kutoka Serikali Kuu ili ziendeshe miradi.”
“Hii tabia imeanza kusambaa, hawa wanamhujumu Mkuu wa nchi ambaye anatafuta fedha za maendeleo usiku na mchana, pia wanaihujumu Halmashauri na kuwahujumu wananchi wa wilaya ya Butiama sababu hii ni kodi yao.”
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumanne, Februari 27, 2024) wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, mkoani Mara.
Amewaeleza watumishi hao mchezo huo unapoanza zinatumika mbinu ambazo Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI wala Katibu Mkuu hawawezi kugundua. Aidha, madiwani wala wakuu wa idara hawawezi kubaini.
“Tarehe 13 Juni, 2022 Mkurugenzi wa Halmashauri aliandika barua kwenda HAZINA kuwajulisha kuwa watakuwa na fedha za ziada Sh. 736,228,732/- ambazo wanaomba kibali ili wazihamishe. Lakini kabla hawajapewa kibali cha sh. milioni 736, Mkurugenzi aliyekuwepo alishaihamisha na wakati anaomba hicho kibali, watu wa fedha wakawa tayari wameshamtumia nyongeza ya sh. milioni 150 na kufanya jumla iwe Sh. milioni 886, naye akazihamisha zote.”
“Hoja inakuja kwamba, kama mliandika barua kuomba kibali cha Sh. milioni 736, ni kwa nini mhamishe zote sh. milioni 886? Kufika Julai 2022, katika kuhamisha fedha ili zirudi Halmashauri, wakatuma sh. milioni 306 lakini walishtuka na haraka walirudisha Sh. milioni 98, zikabakia sh. milioni 208.”
Amesema kiutaratibu, kila mara fedha inapotumwa kutoka serikali kuu, Mweka Hazina wa Halmashauri anapaswa kuwajulisha Mkurugenzi, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkuu wa idara husika. “Na fedha zote huwa zina maelekezo maalum iwe ni ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya, barabara au kituo cha afya lakini fedha hizo zilipoingia, madiwani hawakuambiwa, Mwenyekiti hakuambiwa wala Mkuu wa Idara yoyote hakujulishwa.”
Amesema Mkurugenzi wa Halmashauri aliyekuwepo Bi. Patricia Robi Kabaka alipoulizwa, alisema hana taarifa na uwepo wa fedha hizo. “Je, ni nani kazileta, ni nani aliziomba? Kwenye matumizi ya sh. milioni 208, zilitolewa sh. milioni 151 na kupelekwa kwenye maeneo ambayo tayari yana bajeti. Na hakuna diwani wala mkuu wa idara aliyeambiwa matumizi haya.”
Akitoa mchanganuo wa matumizi hayo, Waziri Mkuu amesema sh. milioni 7 zilitumika kwenyeTASAF, Sh. milioni 35 (sensa ya watu na makazi), sh milioni 18 (AMREF), sh. milioni 75 (kupanga na kupima ardhi), Sh. milioni 4 (marejesho ya mshahara – unclaimed salary) na sh. milioni milioni 12 (ununuzi wa vifaa vya nyumba ya Mkurugenzi).
“Kamanda wa PCCB Mkoa, fuatilia kwa kina na hata ikibidi kumfuata Mkurugenzi aliyepita fanya hivyo. Tunataka tujue ni nani alihusika na yote haya na ilikamilisha, peleka mahakamani wote wanaohusika.”
“Haya matumizi yote ilikuwa ni njia ya kutolea fedha ndiyo maana orodha yake haikupelekwa kwenye Baraza la Madiwani, Kamati ya Fedha haikuhusishwa na wala hakuna Mkuu wa Idara aliyepewa taarifa.”
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Serengeti.
There is noticeably a bundle to know about this. I assume you made certain nice points in features also.