Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Morogoro imemhukumu Mohamed Salange (38) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kike wa kufikia wa miaka 12. Mei 3, mwaka huu, Salange alihukumiwa kifungo kingine cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na kosa la ukatili dhidi ya mtoto wake wa kufikia mwenye miaka tisa.
Katika kesi hiyo alidaiwa kwa nyakati tofauti, alimfanyia ukatili mtoto huyo kwa kumng’oa meno, kumchoma moto sehemu ya juu ya mdomo na kwenye makalio, kumpiga na kumvunjavunja mkono na kuvunja korodani kisha kumtoboa sehemu ya ngozi ya uume wake.
Soma Zaidi:Nini Kifanyike Kupunguza Wafungwa Magerezani?
Jana katika kesi yake ya pili ya ukatili, Salange akisomewa hukumu hiyo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Renatus Barabara amesema Mahakama hiyo imejiridhisha pasipo na shaka kwamba baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji, mshtakiwa anayo kesi ya kujibu.
“Kwa mujibu wa sheria ya 130 (1) kifungu cha 2 (e) na sheria ya 131, kwa kuzingatia uzito wa kosa, umri wa mwathirika, ni dhahiri yako madhara ya kiakili, kifikra ameyapata, hivyo Mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama hizo,” amesema Hakimu huyo.