Baada ya sintofahamu iliyozuka kuhusu uwezekano wa kuondolewa kwa Sanamu la Askari linalopatikana kwenye makutano ya barabara ya Samora na Azikiwe jijini Dar es Salaam kutokana na ujenzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT),
serikali imethibitisha kuwa sanamu hilo halitaguswa wala kuondolewa. Taarifa hizi zilikuwa zikisambaa mitandaoni na kuleta wasiwasi kwa wananchi na wapenda historia.
Sanamu la Askari, lililojengwa mwaka 1927 na utawala wa kikoloni wa Kiingereza, lina umuhimu mkubwa wa kihistoria. Lilijengwa kama kumbukumbu ya mchango wa askari wa Kiafrika waliopigana katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 na 1918. Mnara huu unahifadhiwa na Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333 na Sheria ya Makumbusho ya Taifa, Sura 281, na ulitangazwa kuwa urithi wa taifa kupitia tangazo la serikali No.498 la mwaka 1995.
Ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi wa BRT, ambao unajumuisha barabara kutoka Gongo la Mboto hadi katikati ya jiji, umekuwa ukisababisha mabadiliko makubwa katika miundombinu ya Dar es Salaam. Hata hivyo, mamlaka zimethibitisha kuwa sanamu hili litabaki katika eneo lake la sasa bila kuathiriwa na ujenzi huo.
SomaZaidi;Bashungwa Aweka Wazi Kupunguza Msongamano Katika Majiji
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, TANROADS imesema kuwa mradi wa BRT unaendelea vizuri na lengo ni kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam. Awamu ya tano ya mradi huu pia imeanza, ikilenga kuboresha zaidi mfumo wa usafiri wa umma na kurahisisha harakati za wananchi jijini.
Kwa kuzingatia umuhimu wa kihistoria wa Sanamu la Askari, hatua ya kutokuliondoa inatazamwa kama njia ya kuhifadhi urithi wa kitaifa huku ikiruhusu maendeleo ya miundombinu muhimu kama vile BRT kuendelea. Serikali imesisitiza kuwa inafanya kazi kwa karibu na wataalam wa urithi na historia kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo haileti athari mbaya kwa maeneo ya kihistoria na kumbukumbu za kitaifa.
Hatua hii imetuliza wasiwasi wa wananchi na kuonyesha kuwa inawezekana kubalansi kati ya maendeleo ya miundombinu na uhifadhi wa urithi wa kitaifa, jambo ambalo linapaswa kuigwa na miradi mingine ya maendeleo nchini