Ikiwa ni siku chache tu tangu ifungiwe na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kufanya usajili kutokana na kukiuka kanuni za uhamisho, Klabu ya Yanga imechafua tena faili lake katika shirikisho hilo baada ya kuzuiwa kwa mara ya pili kusajili kutokana na kosa lingine tofauti na lile la awali.
Aprili 12, mwaka huu, TFF ilitoa taarifa kwa umma kuwa FIFA imeifungia Yanga kusajili kutokana na kukiuka kanuni ya uhamisho za kile kilichoitwa Annexe 3 ya Kanuni ya Uhamisho (RSTP) ya shirikisho hilo.
Soma Zaidi:Kunani; TFF na Yanga?
Taarifa hiyo ikieleza kuwa Yanga haikuingiza uthibitisho wa malipo wa uhamisho wa mchezaji husika (ambaye haikumtaja) katika usajili (TMS), licha ya kukumbushwa kufanya hivyo mara kwa mara na kwamba suala hilo lipo mezani kwa Sekretarieti ya Nidhani ya FIFA kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, wakati suala hilo likiwa bado la moto na wadau wa soka wakisikilizia kile ambacho Sekretarieti ya Nidhani ya FIFA, itaamua mbali na adhabu hiyo ya kufungiwa, jana TFF ilipokea taarifa kutoka shirikisho hilo la soka duniani na kuitoa kwa umma kuwa Yanga imefungiwa tena kusajili kutokana na kutolipa malimbikizo ya mishahara pamoja na fidia ya kuvunja mkataba na aliyekuwa mchezaji wao, Mzambia Lazarus Kambole.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, mchezaji huyo raia wa Zambia alifungua kesi FIFA kuitaka Yanga kumlipa malimbikizo ya mishahara yake pamoja na fedha za fidia za kuvunjiwa mkataba wake na klabu hiyo.
TFF ilienda mbali zaidi na kuweka wazi na wao wameifungia Yanga kusajili wachezaji wa ndani mpaka pale watakapomlipa nyota huyo.
Hata hivyo, akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe, alisema uongozi wa klabu hiyo unafanyia kazi madai ya Kambole ili kuweza kumalizana naye.
“Hili suala linamalizwa kiofisi, ni jambo ambalo tayari linafanyiwa kazi kuweza kulimaliza,” alisema Kamwe.
TFF imezitaka klabu za soka nchini kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwamo kufungiwa kusajili.
Kambole alijiunga na Yanga Juni 2022 akitokea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini Yanga waliamua kuachana naye msimu uliopita.