Wakala ya Barabara (TANROADS) na Wakandarasi wanaendelea na kazi ya kurejesha miundombinu ya Barabara ya Lindi – Dar- es Salaam ambayo imeharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi Mha. Emil Zengo ameyasema hayo leo tarehe 5 Mei 2024 alipotembelea na kukagua uharibifu uliotokea katika eneo la Somanga – Mtama.
Amesema kuwa leo majira ya asubuhi maji yamefurika kwa wingi na kuharibu eneo la takribani mita 80 katika barabara ya Somanga – Mtama na kukata tuta la barabara hiyo eneo la Mikereng’ende umbali wa Kilomita 10 kutokea Somanga uelekeo wa Lindi.
Pia imeleta athari katika eneo la Lingaula umbali wa kilomita 12 kutokea Nangurukulu uelekeo wa Lindi
Soma zaidi: Kimbunga “HIDAYA” Chakaribia Pwani ya Mtwara
Amesema kuwa jitihada za Serikali zinaendelea kufanywa ili kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo kutokea upande wa Mkoa Pwani na kutokea Lindi.
Mha. Zengo ametoa wito kwa Wananchi na Madereva kuendelea kuwa na subira kwani Serikali kupitia TANROADS inaendelea kufanya kila linalowezekana kurejesha miundombinu ya barabara hiyo na kuwezesha Wananchi kupata huduma ya usafiri katika barabara kama kawaida.
Daraja la Mbwemkuru linalounganisha Mikoa ya Kusini Lindi, Mtwara na Ruvuma, limesombwa na barabara kuharibiwa na Kimbunga Hidaya kinachoendelea kukumba maeneo ya Ukanda wa Bahari ya Hindi ikiwemo Mikoa ya Kusini.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetangaza mwisho wa Kimbunga Hidaya kuanzia usiku wa saa tano na dakika hamsini na tisa May 4 2024 baada ya vipimo kuonesha kuwa kimbunga hicho kimepoteza kabisa nguvu yake baada ya kuingia Nchi kavu kupitia kisiwa cha Mafia.
MWISHO WA KIMBUNGA “HIDAYA”
Dar es Salaam, 04 Mei 2024 Saa 5:59 Usiku:
Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga “HIDAYA” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 01 Mei 2024. pic.twitter.com/lUeGouPkI9— Tanzania Meteorological Authority (@tma_services) May 4, 2024
Upepo wa Kimbunga Hidaya umeleta athari kwenye miundombinu ya umeme hasa baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Pwani. Hali hii inaweza kuleta madhara kwa watu pamoja na mali zao kwenye baadhi ya maeneo.