Hassan Mwakinyo moja kati ya wanamasumbwi mashuhuri nchini Tanzania anatarajiwa kupanda ulingoni na mpinzani wake Mbiya Kanku toka DR Congo mnamo Januari 27, 2024.
Bondia Hassan Mwakinyo amesema amejiandaa kwa asilimia 98 hivyo kilichobaki ni kupima uzito pekee. Hassan ameongeza kwa kusema kuwa hakuna kitakachomfanya ashindwe kupata ubingwa kwani amekwishajiandaa kila idara na kilichobaki ni kuonyesha uweledi wake ulingoni.
Hata hivyo Mwakinyo amewatoa hofu mashabiki wake kwa kuwataka wajiandae tu kushuhudia jinsi atakavyoonyesha burudani ya kuvutia ya ngumi siku ya mpambano.
Hassan na mpinzani wake wanatarajiwa kukutana kwenye kinyang’anyiro cha mpambano wa ubingwa wa WBO Afrika utakaofanyika Amani Complex Indoor Arena, Zanzibar.
Mapambano mengine yatakayopigwa siku hiyo, ni mpambano kati ya Hussein Itaba na Juma Misumari wa Morogoro, Bakari H.Bakari na Seleman Hamad, Masoud Khatibu atazichapa na Yahaya Khamis, pasipo kusahau mwanadada Zulfa Iddi atakaevaana vikali na mpinzani wake Debora Mwenda.