WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya waliokabidhiwa magari ya usimamizi shirikishi kutoka ofisini na kwenda kuwahudumia wananchi.
Mchengerwa ameyasema hayo leo Desemba 14, 2023 mkoani Arusha, wakati akikabidhi magari 13 kwa ajili ya Usimamizi Shirikishi wa Shughuli za Afya kwa Mkoa wa Arusha magari matano na Manyara magari nane
“Ni lazima viongozi mfanye kazi za kuwatumikia wananchi haswa nyie Waganga Wakuu wa Wilaya mtoke ofisini nendeni field mkasimamie miradi ya Afya, ” amesema Mchengerwa na kuongeza
” Mkakague ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi muwe na taarifa za vituo vyenu na kujua ubora wa huduma na sio kukaa ofisini kusubiria taarifa za kuletewa,”amesema.
Amesema hatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu Waganga wote watakaothibitika kusababisha vifo vya mama na mtoto kwa uzembe wakati vifaa vyote muhimu na miundombinu imeshatolewa na serikali.
“Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshatekeleza wajibu wake ameleta kila kitu, miundombinu bora, vifaa tiba, madawa na sasa ametupatia usafiri huu kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wetu sasa kwanini wewe usifanye kazi nendeni mkahudumie wananchi,”amesema.
Naye, Naibu Katibu Mkuu anayeshulikia sekta ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dk. Wilson Mahera amesema ole wao watumishi wa afya wanaofanya uzembe kwa wagonjwa watachukuliwa hatua.
” Na nyie wahudumu wa afya wenzenu wakichukuliwa hatua halafu nyie mkalalamika kuwa hawakustahili adhabu husika na nyie tutawachukulia hatua haiwezekani mgonjwa anataka huduma za afya halafu mnazembea na kupelekea vifo, “amesema Mahera
Waziri Mchengerwa anaendelea na ziara ya Kikazi kwenye mikoa ya Singida, Shinyanga, Kagera, Mwanza na Geita.