Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha adhabu ya kumsimamisha kuhudhuria vikao 15 mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kwa kosa la kumtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa kulidanganya Bunge kuhusu suala la uagizaji wa sukari kutoka nje.
Hatua hii ilifikia baada ya ripoti ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, iliyoongozwa na Mwenyekiti Ally Makoa, kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mpina alikiuka sheria na taratibu za Bunge kwa kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwa Spika na kisha kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu maudhui ya nyaraka hizo. Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alibainisha kuwa kitendo cha Mpina kilikuwa ni cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na kwa Spika mwenyewe. Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, sura 296, kinakataza kumkosea heshima Spika, na kifungu cha 34 (g) kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa za Bunge bila kibali
Tuhuma dhidi ya Mpina zilianza mnamo Juni 4, 2024, wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
SomaZaidi;Spika Aamuru Mbunge Mpina Ahojiwe
Waziri Bashe alieleza kuwa viwanda vya sukari nchini vilivyopaswa kuagiza sukari kutoka nje vilishindwa kutimiza wajibu huo, hali iliyosababisha uhaba wa sukari na kupanda kwa bei hadi Sh10,000 kwa kilo moja. Mpina alipinga vikali kauli hiyo akisema kwamba serikali yenyewe ndiyo kikwazo na sio viwanda vya sukari
Mpina alipewa siku 10 na Spika kuwasilisha ushahidi wake kuhusu madai ya Bashe. Mpina aliwasilisha nyaraka za ushahidi pamoja na vielelezo vingine akidai kwamba Waziri Bashe alisema uongo mara 18 bungeni ili kufanikisha malengo yake binafsi. Pia, alihusisha Waziri Bashe na uagizaji holela wa sukari ambao alisema unalenga kuua kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari nchini
Baada ya majadiliano, Kamati ya Maadili ilipendekeza adhabu ya kusimamishwa kwa vikao 10, lakini wabunge walipendekeza kuongeza vikao hivyo hadi 15. Spika Tulia Ackson alikubaliana na mapendekezo hayo na kutangaza kwamba adhabu hiyo itaanza kutekelezwa mara moja, kuanzia Juni 24, 2024. Hii ina maana kwamba Mpina hatarudi bungeni hadi kikao cha pili cha Bunge cha Novemba 2024
Hatua hii imeibua hisia tofauti miongoni mwa wabunge na wananchi, huku wengine wakiona kuwa ni onyo kwa wabunge wengine kuheshimu taratibu na sheria za Bunge. Hata hivyo, wapo wanaomuunga mkono Mpina kwa hatua yake ya kuibua masuala mazito yanayohusu maslahi ya taifa, wakimtaja kuwa ni kiongozi shupavu anayeweka maslahi ya wananchi mbele