Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi, Aisha Amour amemwagiza mkandarasi anayejenga barabara ya mzungumzo jijini Dodoma kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba, kutekeleza maagizo anayopewa na viongozi wakati wa ukaguzi wa miradi.
Alitoa maagizo hayo leo jijini Dodoma wakati akikagua mradi wa ujenzi huo kwa kiwango cha lami wenye urefu wa km 112.3 sehemu ya Barabara ya Ihumwa Dry Port- Matumbulu – Nala yenye urefu wa km 60.
Pamoja na mambo mengine, Balozi Aisha alimtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia ubora wa kila tabaka kabla ya kuendelea na tabaka lingine, kupima mali ghafi za ujenzi, kuhakikisha ubora kabla ya kuzitumia ili kuzuia barabara hiyo kuharibika kabla ya wakati.
“Hakikisheni mnatumia maabara vema na mkandarasi ahakikishe vifaa vyote vya maabara vinakuwa eneo la ujenzi kipindi chote cha utekelezaji wa mradi” alisema Balozi Aisha.
Pia, aliwataka kuhakikisha wanapambanua mapungufu hayo na kuweka mkakati wa kuyafanyia kazi kwa wakati ili kuleta matokeo chanya.
Aidha, amewataka kufanya kazi kwa kizingatia misingi, kanuni na sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa maeneo ya kazi.
“Hakikisheni wafanyakazi hawajiingizi katika vitendo vya rushwa kwa kupunguza mianya ya rushwa nyakati zote wakati mradi unatelelezwa” alisisitiza Balozi Aisha.
Mradi wa mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma wenye urefu wa km 112. umegawanywa katika sehemu mbili za utekelezaji ukijumuisha Sehemu ya kwanza ya Nala – Nyeyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port (km 52.3) ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 76 na Sehemu ya pili ya Ihumwa Dry Port- Matumbulu – Nala (km 60) ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 60.