Serikali imepanga kuziunganisha Wilaya za Misenyi na Bukoba Vijijini kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kyaka – Katoro – Kanazi hadi Kyetema yenye urefu wa kilometa 60.7 kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa za kiuchumi na uwekezaji ndani ya Mkoa wa Kagera.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Machi 28, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Katoro na Ibwera Katika Halmashuri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini Mkoani Kagera mara baada ya kukagua barabara hiyo.
Bashugwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa kuanza na kilometa 10 kuanzia Kanazi hadi Kalonge pamoja na ujenzi wa daraja kubwa la Kalebe.
“Tunafahamu wananchi mmesubiri lami kwa muda mrefu, Serikali imewasikia na hatua iliyopo sasa ni kumtafuta Mkandarasi mwenye uwezo ili ajenge barabara hii na wakati wa ujenzi tumeona lile daraja la Kalebe tusiliondoe wakati lami inajengwa Mkandarasi atajenga Daraja lingine kubwa pembezoni”, amefafanua Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Kagera kuanza hatua za usanifu wa kipande cha pili cha barabara hiyo kuanzia Kalonge – Katoro (km 26) na cha tatu kutoka Katoro hadi Kyaka (km 24.7) wakati awamu ya kwanza ya ujenzi unaendelea.
Bashungwa ameeleza kuwa Dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa Mkoa wa Kagera ni kuwa na uchumi wa uhakika wa kile kinachozalishwa kufika kwenye masoko kwa kuunganisha mawasiliano ya barabara na bandari mbili kubwa za Bukoba Mjini na Kemondo ambazo hivi sasa zipo kwenye maboresho makubwa.
Vilevile, Bashungwa amemuagiza Meneja wa TANROADS kukamilisha haraka na kuwasilisha tathimini ya uhakiki wa wananachi watakaopisha ujenzi wa barabara hiyo ili Serikali iweze kutoa malipo ya fidia kwa wakati.
Hatahivyo, Bashungwa amepokea ombi la Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini la kupata daraja la chuma katika Mto Kyenyabasa ili kusaidia wananchi kuwa na usafiri wa uhakika na salama katika usafirishaji wa abiria na mizigo kuingia Bukoba Mjini na kuahidi ndani ya miezi miwili TANROADS watakiwa wameshafunga daraja hilo.
Naye, Mbunge wa jimbo la Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza amesema kilio kikubwa cha wananchi ni kupata barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni barabara muhimu ya kiuchumi, kijamii na kiusalama pia ndiyo inaunganisha Wilaya ya Bukoba Vijijini na nchi jirani ya Uganda kupitia Misenyi ambapo biashara kubwa zinafanyika.