Bodi ya Chuo Kikuu cha Howard, kihistoria kinachotambuliwa kuwa chuo kikuu cha watu weusi huko Washington DC, imeazimia kumvua Sean “Diddy” Combs shahada yake ya heshima.
Tangazo hilo linakuja baada ya CNN kuchapisha video ya CCTV ya mtayarishaji huyo wa muziki wa hip-hop akimpiga mpenzi wake wa zamani kwenye ukumbi wa hoteli.
Katika taarifa siku ya Ijumaa, chuo kikuu kilisema “tabia yake kama ilivyonaswa kwenye video iliyotolewa hivi karibuni haiendani kabisa na maadili na imani kuu za Chuo Kikuu cha Howard kiasi kwamba inachukuliwa kuwa hafai tena kushikilia heshima ya juu zaidi ya taasisi hiyo.”
Rapa huyo aliomba msamaha baada ya video hiyo kutolewa mwezi uliopita kwa shambulio dhidi ya mwimbaji Cassandra “Cassie” Ventura. “Nilichukizwa nilipofanya hivyo. Nimechukizwa sasa,” Bw Combs alisema katika taarifa yake.
“Nilikwenda na nikatafuta usaidizi wa kitaalamu. Niliingia kwenye matibabu, kwenda kwa wataalamu wa kurekebisha tabia. Ilinibidi kumwomba Mungu rehema na neema yake. Ninaomba radhi sana.”
Chuo Kikuu cha Howard kilimkabidhi Bw.Combs shahada hiyo mwaka wa 2014. Kilisema katika taarifa yake kwamba kitasitisha ufadhili wa masomo kwa jina lake na kusitisha “mkataba wa zawadi” wa 2016 na rapa huyo.
Makubaliano hayo yalikuwa mchango wa $1m (£785,000) ambao alitoa kupitia taasisi yake.
Sean Combs Foundation haijasema chochote kuhusu hatua hiyo.
Taarifa ya chuo kikuu ilisema jina la Bw Combs litaondolewa kwenye hati zote zinazoorodhesha waliopokea shahada ya heshima.
“Chuo kikuu hakiyumbishwi katika kupinga vitendo vyote vya unyanyasaji kati ya watu,” ilisema taarifa hiyo.
Wanawake wanne, akiwemo aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu Bi Ventura, wamefungua kesi dhidi ya mwanamuziki huyo, wakimtuhumu kwa unyanyasaji wa kingono na kimwili.
Kesi ya Bi Ventura ilitatuliwa mnamo Novemba, na Bw Combs amekanusha madai yote ya unyanyasaji wa kijinsia. Katika taarifa iliyotolewa Desemba mwaka jana, Bw Combs alijitetea dhidi ya kile alichoeleza kama “madai ya kuudhi” yaliyotolewa na “watu wanaotafuta malipo ya haraka”. “Niseme wazi kabisa: sikufanya jambo lolote baya lililodaiwa,” alisema na kuongeza kuwa atapigana kusafisha jina lake.