Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Beatrice Elias (36), mkazi wa Mtaa wa Katanini Wilaya ya Moshi kwa tuhuma za kumuua mumewe, Ephagro Msele (43) kwa madai ya kumkuta kwa mzazi mwenzake.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na Msele, Mei 25, 2024, Beatrice baada ya kutoka msibani alikokuwa na mumewe, alimfuatilia kila anapokwenda kwa kutumia usafiri wa bodaboda na baada ya mumewe kuegesha gari lake mahali, alidaiwa kwenda nyumbani kwa mwanamke aliyezaa naye.
Inadaiwa kuwa, Beatrice alipofika nyumbani kwa mwanamke huyo, Kitongoji cha Pumuani A, alijificha getini na baadaye aligonga geti na mumewe ndiye aliyetoka kumfungulia.
Read More:Frateri Aliyejinyonga Azikwa Kimya Kimya
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kukutana getini, yaliibuka mabishano kati yao, ndipo Beatrice alipofanikiwa kutekeleza tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amedai leo Jumapili Mei 26 kuwa, Beatrice alimvizia mumewe akitoka nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumchoma na kitu chenye ncha kali.
“Ni kweli kumetokea hili tukio, usiku wa Mei 25, 2024 saa 3:50 usiku katika Kitongoji cha Pumuani A, Kata ya Kirua Vunjo, mtu aliyejulikana kwa jina la Ephagro Msele, mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Katanini, Kata ya Karanga, aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya mgongoni,” amesema Kamanda Maigwa.