Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Abdulrahaman Kinana amesema Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA) wamepata uhuru mkubwa wa kufanya maandamano nchi nzima lakini bado wamekituhumu chama cha mapinduzi na serikali kwa mambo ya uongo hayo yamejiri leo, Jumapili Mei 05.2024 alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho mkoa wa Dodoma.
“Kwa muda wa wiki kadhaa ndugu zetu wa chama cha CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) walipata uhuru mkubwa sana, kufanya maandamano, kufanya mikutano ya hadhara, kuzunguka sehemu mbalimbali nchini, na katika mizunguko yao wamezungumza mambo mengi, wametutuhumu wanachama wa CCM, wameituhumu serikali ya CCM (Chama cha Mapinduzi), wamemtuhumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa) kwa mambo ya uwongo, hatukatai kukosolewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzushiwa wala kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo au ya uwongo” -Kinana
Soma zaidi:Untold story over CCM-CHADEMA reconciliation talks
“Kubwa walilofanya katika mizunguko yao ambao wao wanadhani ni mtaji mkubwa sana ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mfarakano miongoni mwa Watanzania, hiyo ndio ilikuwa ajenda yao kubwa, wakaenda mbali zaidi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuligeuza kuwa ajenda yao ya uchaguzi kuanzia sasa mpaka 2025 kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Rais Mzanzibar ambaye anataka kuihujumu upande wa huu wa Tanzania Bara (Tanganyika) kwenye Muungano, wanataka Watanzania waaminishwe wajenge chuki juu yao ili iwe ajenda yao ya ushindi, nadhani wameshindwa” -Kinana