Serikali ya Tanzania imejizatiti kuweka mkazo wa kipekee katika kuendeleza vijijini kama njia ya kuchochea uchumi jumuishi nchini. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,
Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, alisisitiza hili wakati wa kupitisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/2025 na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Prof. Mkumbo alieleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya vijijini kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Alisema kuwa ongezeko la mtandao wa barabara za vijijini ni hatua muhimu katika kufanikisha maendeleo ya maeneo hayo. “TARURA imefanikiwa kuongeza kiwango cha barabara za changarawe kutoka kilomita 24,493 mwaka 2020 hadi kufikia kilomita 41,107 mwaka 2024, zaidi ya lengo letu la kilomita 35,000 ifikapo mwaka 2025,” alisema Prof. Mkumbo.
Waziri huyo aliongeza kuwa upanuzi wa mtandao wa barabara vijijini utasaidia sana katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, na uvuvi kutoka vijijini hadi sokoni. “Tukishakuwa na mtandao wa barabara vijijini, itasaidia wananchi kuweza kufanya biashara, kusafirisha mazao yao na kujipatia kipato,” alisisitiza Prof. Mkumbo.
SomaZaidi;Bil.18.5 Kutumika Ujenzi wa Mifereji ya Maji Tabora
Pamoja na ongezeko la barabara za changarawe, Serikali pia imeongeza kiwango cha barabara za lami kutoka kilomita 2,205 mwaka 2020 hadi kilomita 3,224 mwaka 2024. Prof. Mkumbo alieleza kuwa miradi inayoendelea itasaidia kuongeza zaidi kiwango hicho. “Tunaamini kuwa hatua kubwa zaidi zitapigwa kwa miradi inayoendelea,” aliongeza.
Aidha, Serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha kuwa maendeleo haya yanakuwa endelevu na yanafikia wananchi wengi zaidi vijijini. Prof. Mkumbo alihimiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali katika kufanikisha malengo haya. “Serikali inajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kuwa maendeleo haya yanafikia wananchi wengi zaidi vijijini, na tunahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kufanikisha hili,” alisema.
hatua hizi za Serikali zinaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia TARURA. Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa malengo ya maendeleo vijijini yanafikiwa kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora za miundombinu.