Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameeleza kuwa, ziara aliyofanya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko mkoani Mtwara Novemba 14 na 15, 2023 imeleta matokeo chanya kwani maagizo yote aliyoyatoa yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo mitambo ya umeme ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa muda mrefu sasa imeanza kuzalisha umeme.
Amesema hayo wilayani Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa mauziano ya gesi asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma kilichopo mkoani Mtwara na uwekaji saini hati ya makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa Teknolojia ya Miundombinu Midogo ya Kubadilisha Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Mini-LNG
Amesema kuwa, Dk Doto Biteko akiwa mkoani Mtwara alifanya ziara katika kituo cha umeme mkoani humo na kukuta mitambo miwili ya umeme haifanyi kazi kwa muda mrefu ambapo alitoa agizo kwa TANESCO kuhakikisha mitambo hiyo inatengemaa na kuanza kuzalisha umeme ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme.
Ameeleza kuwa, kutokana na agizo hilo la Dk Biteko, mitambo hiyo imefanyiwa ukarabati na sasa inafanya kazi na kuongeza megawati 6.5 kwenye mzunguko.
Ameongeza kuwa, kazi ya ujenzi wa eneo ambalo litawekwa mtambo mwingine wa megawati 20 mkoani humo unaendelea kwa kasi kubwa hali itakayozidi kuimarisha hali ya umeme na kuchochea uwekezaji.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake na hii inajumuisha maagizo aliyoyatoa wakati alipofanya ziara yake katika Kisiwa cha Songosongo ambapo aliagiza masuala mbalimbali ikiwemo ya wananchi kupatiwa usafiri wa uhakika utakaowawezesha kuvuka maji kwenda wilayani Kilwa na pia kusambaziwa na kupatiwa umeme wa uhakika.
Source :Habari Leo