Kaimu kocha mkuu wa klabu ya Simba, Juma Mgunda, amefichua kile ambacho amekifanya kwa wachezaji wake ambao sasa wamekuwa wakipambana uwanjani na kupata matokeo mazuri kwenye michezo yao ya Ligi kuu.
Mgunda amesema kuwaweka wachezaji wake karibu na kuongea nao kama mzazi kumesaidia kubadili upepo wa wachezaji wake na kupambana kumpatia matokeo mazuri kwenye michezo minne aliyoisimamia timu hiyo tangu kuondoka kwa kocha Mkuu Abdelhak Benchikha.
Katika michezo hiyo minne ambayo Mgunda amesimama kama kocha mkuu wa Simba, amepata ushindi kwenye michezo mitatu na kupata sare moja.
Also Read:Simba Sets Record For Worst Results
Mgunda alianza kwa sare ya bao 2-2 dhidi ya Namungo, akapata ushindi wa mabao 2-0 kwenye michezo dhidi ya Mtibwa Sugar na Tabora United kabla ya juzi kuifunga Azam FC mabao 3-0.
Mgunda alisema amekuwa akiongea na wachezaji wake wote na kuwakumbusha umuhimu wa michezo iliyobakia na kuwataka kupambana kwa ajili ya timu bila kuangalia jambo lolote.
“Nashukuru wananisikiliza, nimekuwa nikiongea nao kama mzazi, huwa nawaambia kila mchezaji aliyesajiliwa na timu hii ana wajibu wa kucheza na kuitumikia, hii imesaidia hata wale ambao walikuwa hawapati nafasi ya kucheza, nikiwapa nafasi wananipa matokeo chanya,” alisema Mgunda na kuongeza,
“Mfano mchezo wa jana (juzi) dhidi ya Azam, nilikaa na wachezaji na kuwakumbusha umuhimu wa mchezo huo, bahati nzuri na wenyewe walikuwa wanaitaka sana hii mechi, niliwaambia hii mechi ni muhimu sana kushinda kwa sababu itatupa kitu kuelekea kwenye michezo yetu ya mwisho, na wote tumeona kile wachezaji wangu walichokifanya.., kwa kweli nawapongeza sana,” alisema Mgunda.
Alisema anajivunia wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi lakini kwa sasa kila anayempa nafasi anaenda kufanya kazi kubwa kwa ajili ya timu.
“Kwa sasa tunaangalia michezo inayofuata, tunashukuru kwa ushindi dhidi ya Azam, naamini tutaendelea kufanya vizuri kwenye michezo iliyobakia ili tuone mwisho wa ligi tutakuwa kwenye nafasi gani,” alisema Mgunda.
Ushindi wa juzi umeifanya Simba kufikisha pointi 56 ikiwa ni pointi moja nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 68, hata hivyo Simba ipo nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya Azam na michezo miwili dhidi ya Yanga.