Mbunge wa Kawe, Mchungaji Josephat Gwajima, ametoa wito kwa serikali kuanzisha mpango wa maendeleo wa taifa unaotokana na mipango ya wizara zote, badala ya kutegemea kamati moja inayokusanya maoni kutoka kwa wananchi.
Pendekezo hili linakuja katika harakati za kuboresha uratibu na utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini.
Gwajima, akizungumza bungeni, alisisitiza umuhimu wa kuwa na mpango shirikishi ambao unajumuisha mikakati ya kila wizara, ili kuhakikisha kwamba mipango ya serikali inalingana na mahitaji ya maendeleo ya kitaifa. Alisema kuwa kwa sasa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Hali ya Uchumi husomwa siku moja na Bajeti Kuu ya Serikali, jambo ambalo linawanyima wabunge nafasi ya kuchambua na kujadili mikakati ya wizara kabla ya kuanza kuwasilisha bajeti zao.
“Mpango wa Maendeleo na Hali ya Uchumi usomwe mapema bungeni kabla ya wizara hazijaanza kuwasilisha bajeti zao,” alisema Gwajima. “Hii itawapa nafasi wabunge kujiridhisha na kuhoji mikakati ya wizara kama inasoma na Mpango wa Maendeleo wa Serikali.”
Pendekezo hili linakuja wakati ambapo Tanzania inajaribu kuboresha uratibu wa mipango ya maendeleo kwa kuanzisha Tume ya Mipango itakayoratibu na kusimamia masuala yote ya mipango ya maendeleo nchini. Tume hii, ambayo itaongozwa na Rais na wajumbe watakaochaguliwa, inalenga kuhakikisha kwamba mipango ya serikali inatekelezwa kwa ufanisi.
SomaZaidi;Mbunge Waitara Akataa Ushoga Bungen
Mbunge huyo alieleza kuwa Tume ya Mipango inahitaji kuwa na ulinzi thabiti wa mipango ya muda mrefu ya taifa na kuhakikisha ilani za uchaguzi za vyama zinaendana na mpango wa taifa, ili kuhakikisha utekelezaji wake unaleta manufaa kwa wananchi
Gwajima aliongeza kuwa, “Ni muhimu ilani za uchaguzi za vyama zikakaguliwa na Tume ya Taifa ya Mipango kusudi chama kikiingia madarakani kiweze kutekeleza mpango husika. Hii itahakikisha uwiano kati ya ilani za uchaguzi na mpango wa taifa.”
Kupitia pendekezo hili, Gwajima anatarajia kuona mabadiliko makubwa katika njia serikali inavyoratibu na kutekeleza mipango yake ya maendeleo, na hivyo kuleta maendeleo endelevu kwa taifa. Wabunge wengine pia wameunga mkono wazo hilo, wakisisitiza umuhimu wa uratibu na uwiano katika mipango ya maendeleo ili kufanikisha malengo ya kitaifa