Katika kikao cha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2024/25, Mbunge wa Viti Maalum Khadija Shaaban Taya amesimama mbele ya Bunge na kutoa hoja ya dhati kuhusu hali ya maadili katika tasnia ya sanaa nchini Tanzania.
Katika hotuba yake yenye uzito, ameomba serikali kuchukua hatua madhubuti katika kurejesha utu na maadili miongoni mwa wasanii. “Mazingira ya sasa katika tasnia ya muziki yamejaa lugha chafu na matusi, na hili linatia wasiwasi mkubwa,” amesema Khadija Shaaban Taya. ”
Nyimbo zetu zimejawa na maneno yenye matusi na lugha ya ajabu ambayo haifai kusikilizwa na watoto wetu. Wasanii wanatumia jukwaa lao kufanya propaganda ya lugha chafu na kuathiri maadili ya kizazi kichanga.” Amezungumzia jinsi viongozi wa tasnia, kama vile Babu Tale, wanavyoshindwa kusimamia maadili na kutoa mwongozo unaofaa kwa wasanii.
SomaZaidi;Usanga Katika Tuzo Za Albamu Bora 2023
“Babu Tale, ambaye ni Msimamizi wa karibu wa wasanii, anashindwa kutetea maadili. Anaposikiliza nyimbo zenye lugha chafu, hawaambii kuwa hazina matamshi mazuri. Na kwa kusikitisha, hata nyumbani kwake, muziki wa aina hiyo haupewi nafasi, lakini watoto wetu mitaani wanaweza kuharibika kwa sababu ya muziki unaotolewa sasa.” Mbunge huyo ameonya kuwa hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa haraka ili kurejesha utu na maadili katika tasnia ya sanaa.
Ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kufanya kazi kwa karibu na wadau wa sekta hiyo ili kuanzisha mikakati thabiti ya kudhibiti matumizi mabaya ya lugha na kukuza utamaduni unaofaa kwa jamii. Pamoja na hayo, ametoa wito kwa jamii nzima kushirikiana katika kuhamasisha maadili mema na kuelimisha vijana juu ya madhara ya kutumia lugha chafu na matusi katika kazi za sanaa. Amesisitiza umuhimu wa kujenga jamii inayojali na inayoheshimu utu na maadili, kwa kuwa kizazi kichanga ni msingi wa taifa lenye mafanikio na heshima ulimwenguni.