Siku tatu baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa ripoti ya hali ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na magonjwa ya zinaa, Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imeizungumzia ripoti hiyo, ikitaja ugumu inaokabiliana nao katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU nchini.
Mei 21, mwaka huu, WHO ilitoa ripoti ikionyesha UKIMWI bado haujapungua duniani, huku zaidi ya watu milioni moja wakiambukizwa kila mwaka magonjwa ya zinaa, yakiwamo kaswende na kisonono.
Jana, katika mazungumzo mahsusi na Chombo Kimoja cha habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TACAIDS, Dk. Jerome Kamwela, aliorodhesha mambo manne yanayokwamisha jitihada za kukabiliana na janga hilo nchini.
Soma Zaidi:Rising Hepatitis Infections Prompt Urgent Community Education
Alitaja vikwazo hivyo ni hali ngumu ya uchumi kwa wanawake inayowasukuma kurubunika kirahisi na kuingia kwenye ngono zembe na usiri miongoni mwa wenza kushindwa kuwaeleza wenzao hali zao kiafya hata baada ya kutambua wana maambukizi.
Dk. Kamwela alitaja kikwazo cha tatu ni unyanyapaa katika jamii dhidi ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU), unaochagiza hofu ya kupima kutambua hali ya kiafya.
Kikwazo cha nne, kwa mujibu wa Dk. Kamwela, ni nchi kuendelea kutegemea wafadhili kutoka nje, jambo analolitafsiri ni hatari na kushauri serikali kuwekeza fedha za ndani kuwanusuru wananchi dhidi ya janga hilo.
MAAMBUKIZI YAPUNGUA
Hata hivyo, Dk. Kamwela alisisitiza kuwa maambukizi mapya yameendelea kupungua mfululizo kwa zaidi ya asilimia 50.
“Mwaka 2010 tulikuwa na karibu watu 110,000 wanaopata maambukizi kila mwaka. Sasa hivi tumesema tuko kwenye 60,000. Hata vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa zaidi ya theluthi mbili.
“Unyanyapaa miaka 10 iliyopita tulikuwa tuna asilimia 25, sasa hivi tuna asilimia tano. Tunaendelea kupata faida. Pamoja na mafanikio haya, kuna changamoto za makundi,” alisema.
Dk. Kamwela alisema kwenye malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 yako malengo matatu, mawili wanayafikia na moja lenye changamoto ni kutambua watu wanaoishi na VVU.
“Kwenye mafanikio, mengine tuliyo nayo ni kuendelea kupunguza maambukizi mapya na kuendelea kupunguza vifo vinavyotokana na UKIMWI na kuendelea kupunguza unyanyapaa.
“Changamoto, maambukizi yameendelea kutokea na kuna shida kwenye makundi, moja ni kundi la vijana wanaochangia theluthi moja ya maambukizi mapya, walioko shuleni, vyuoni na mitaani. Kundi ambalo tunafikiri linahitaji kufikiwa kwa karibu.
“Tuna makundi maalumu, watu ambao wanaofanya kwa mfano, biashara za ngono, wanaotumia dawa za kulevya, wanaofanya kazi za kuhamahama mfano, madereva wa masafa marefu, wavuvi, wanaoishi kwenye visiwa. Haya ni makundi ambayo yanafanya ile kasi ya kupunguza maambukizi mapya iwe ngumu, alisema.
Pia alisema hata kupata huduma za tiba ili wafubaze virusi ni ngumu kwa sababu ni watu ambao wanatoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Tunajaribu kuzifanya programu zetu kufikia makundi haya kulingana na utofauti wao. Pia kuna watu wanaofanya kazi kwenye migodi midogo ya madini isiyo rasmi. Yako maeneo hayo kweli tunaona tunahitaji kufanyia kazi,” alisema,
Alisema hayo ndiyo makundi makubwa muhimu ambayo hawajayafikia na wanafikiri kwa kipindi kilichobaki cha sasa hadi ifikapo 2030 kwa kutumia nguvu zao na serikali na sekta binafsi na wadau wa maendeleo, miradi yao inayowalenga inaweza kuonesha mafanikio chanya.
HALI KWENYE FAMILIA
Dk. Kamwela alisema jambo kubwa wanaliona katika familia ni unyanyapaa, ambapo bado suala la uwazi juu ya masuala ya UKIMWI ni tatizo.
Alisema kuna familia ambazo mwenza mmoja anaishi na maambukizi na mwezake asijue na ziko ambazo mtoto anaweza kupata maambukizi familia ikaona ni shida isiwaambie watu ili wamsaidie na kumlinda.
“Kuna kesi za unyanyapaa, unyanyasaji wa kijinsia. Watoto wanabakwa na ndugu wa familia na hayo mambo yanazungumzika tu ndani ya familia hayachukuliwi hatua za kisheria.
“Haya yote ndiyo tunaona kwenye familia zetu tunatakiwa kuongeza nguvu. Kuelimisha familia zetu ili waone kuna mambo yakitokea waone mtu akipata maambukizi ni kama ugonjwa mwingine, asaidiwe kupelekwa hospitalini akapimwe, apewe tiba na akirudi asinyanyapaliwe asaidiwe.
MAENEO YANAYOWEKEWA NGUVU
“Vinapotokea vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au vingine vyenye matukio hasi ambavyo ni sehemu ya mila potofu kama kukeketa watoto, ndoa za utotoni.
“Ninafikiri ni miongoni mwa maeneo ambayo kwa sasa tunayawekea nguvu zaidi, katika ngazi ya familia kwa sababu yanatokea ndani ya familia ambapo si rahisi kuyajua na kuchukua hatua stahiki,” alisema.
Katika mpango ho, alisema wanashirikiana na wadau wao wa maendeleo kuhakikisha wanachangia utaalam, rasilimali za kutekeleza afua, sekta ya umma ikiwamo Wizara ya Afya kuhakikisha huduma zinafika kila mahali ili jamii izifikie.
Pia alisema wanashirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha kwenye mihadhara yao wanatoa elimu ya kupunguza unyanyapaa, watu wawe jasiri wanapojikuta na maambukizi ili wakapate huduma stahiki.
Kadhalika, alisema katika sekta usafirishaji barabara kutoka Dar es Salaam- Tunduma njiani wameweka vituo kwa ajili ya kutoa huduma kwa waendesha magari masafara marefu zaidi wanakolala ili wapate elimu na huduma.
Pia alisema wanashirikiana na sekta binafsi kwa kuwa ndiyo inaajiri sana, kuhakikisha huduma za kinga zinakuwapo mahali pa kazi na pia, kuwalipia watumishi wao wanaohitaji matibabu na huduma zingine za afya.
“Hatusemi hatujakwama, kama nilivyokuonesha matokeo tuliyopata na mafanikio yetu tunaendelea bado kuhakikisha nguvu za wadau wote tunazitekeleza na kufikia malengo tuliyojiwekea.
Hata hivyo, alisema changamoto ni kwamba mahitaji ya huduma kwa nchi ni makubwa kuliko uwezo na suala la rasilimali fedha, ambayo ni kazi ambayo tume inashirikiana na wadau wa maendeleo na serikali kuhakikisha afua za UKIMWI zinafadhiliwa kwa kiwango kinacholeta tija.
MAKUNDI HATARISHI
Dk. Kamwela alisema vijana ni nguvu kazi ya nchi, lakini wana madhaifu na wengi hawajajenga nguvu za kiuchumi, tegemezi, wapo katika ngazi mbalimbali za elimu.
Alisema kundi hilo kama halipati elimu ya kutosha ya kujikinga, watu wazima wenye nguvu za kiuchumi ni rahisi kuwarubuni kwenye ngono, ndio maana wana mchango wa theluthi moja ya maambukizi mapya.
“Kina mama nao ni vivyo hivyo, mila na desturi zetu zinafanya wasiwe na nguvu ya uchumi, wasiwe na uwezo wakutoa uamuzi yanayohusu hata saa nyingine yanayohusu afya zao.
“Inabidi wasubiri au waombe ruksa kwa wenza wao ambao ni wanaume. Pia takwimu zinaonesha mzigo mkubwa wa mama upo kwa kina mama na wasichana, ndio maana serikali inaangalia sana masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na mila potofu. Hili ni eneo ambalo sisi tunasema linahitaji kuangaliwa upya ili kuwa na miradi mikubwa,” anashauri.
Alisema kuna mradi wa wasichana malehe ambao umesaidia vijana wa kike na wanawake vijana ambao hawana nguvu za kiuchumi na wapo katika hatari ya kupata maambukizi kuweza kupata elimu.
Hata hivyo, alisema kama mtaalam yote hayo wakitaka kuyapunguza kwa haraka ni kuwezeka kuzuia maambukizi kundi la hilo.
Pili, alisema kuondoa vikwazo vinavyofanya kundi hilo lishindwe kupata huduma na kujikimu kiuchumi na kutegemea kufanya biashara hatari za kuwaweka kupata maambukizi.
Alitaja jambo la tatu ni kushawishi sekta binafsi kusaidia kuwekeza katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
“Mapambano hayawezi kuwa endelevu kama wataendelea kutegemea ufadhili kutoka nje. Sasa hivi kama watanzania tuchukue jukumu la kuwekeza katika kuwakinga raia wetu,” alishauri.
Alitolea mfano sehemu za starehe kuwa kundi kubwa linalotoa huduma ni vijana wa kike na vijana wanawake, hivyo lazima wawakinge lisitumbukia katika ngono zembe.
EAC NA SADC
Alisema asilimia 90 ya mzigo wa UKIMWI duniani upo kwenye nchi za Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika.
“Tunafikiri Tanzania tuko vizuri tukijilinganisha na wenzetu, hali yetu ni nzuri na kitakwimu tunafikiri tutafikia malengo na tulishatajwa miaka miwili iliyopita tulikuwa kati ya nchi tano za Afrika zilizotimiza malengo,” alisema.
I’m really impressed with your writing skills as well as with the layout on your weblog. Is this a paid theme or did you modify it yourself? Either way keep up the excellent quality writing, it’s rare to see a nice blog like this one today..