Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amesema anakerwa na tabia iliyozuka katika hospitali na vituo vya afya kuuza kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kinyume cha Sera ya Afya.
Kutokana na hali hiyo amepiga marufuku tabia ya watumishi katika kada hiyo muhimu kuuza kadi hizo.
Ummy alibainisha hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya ugawaji wa vitabu vya kufuatilia maendeleo ya mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano, iliyofanyika kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.
Also Read:Serikali Yadhamiria Kuboresha Huduma za Ukunga
“Kuna jambo ambalo linanikera sana. Hivi sasa kadi za kliniki kwa ajili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hazipatikani. Wanasema hazipo lakini kadi zinauzwa na sera inasema kadi ni bure. Nasisitiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya sitaki kusikia mjamzito anauziwa kadi ya kliniki.
“Mjipange leo hapa tunagawa kadi milioni 1.2 lakini kwa mwaka makadirio ya mahitaji ya kadi ni milioni 1.4. kati ya bidhaa ambazo sitaki kusikia haipatikani ni kadi hizi za kliniki kama nilivyoelekeza kwenye upatikanaji wa damu hata kama bajeti itatoka kidogo mhakikishe kadi zinakuwapo za kutosha. Moja ya vitu vya kipaumbele ni kadi za wajawazito na watoto chini ya miaka mitano,” alisisitiza.
Pia alisema waganga wakuu lazima wafuatailie usambazji wa kadi pamoja na makisio yao ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kwa mwaka.
Akizungumzia kuhusu hali ya wajawazito kuhudhuria kliniki, alisema kwa hivi sasa asilimia 80 ya wanaenda kliniki angalau mara nne katika kipindi chao cha ujauzito.
“Lakini bado hatufanyi vizuri kwa kuwa mahudhurio ya kwanza ni asilimia 41 tu ndiyo wanahudhuria chini ya wiki 12 au miezi mitatu tangu kupata ujauzito. Twendeni tukahamasishe kinamama kwenda kliniki mapema.
“Ukiwahi kuna changamoto ya kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi unazipunguza, hivyo kama mama mwezi wa kwanza hujaona wageni (hedhi), wa pili hujaona wageni, basi nenda kliniki utafanyiwa vipimo na kama mjamzito utaanza kliniki mapema,” alisema.
Kadhalika, alisema upatikanaji wa vitabu vya kliniki kwa ajili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano utatumika kuwapima utendaji wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya pamoja na yule wa Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Naelekeza mjipange vizuri kuhakikisha vitabu hivi vinapatikana mapema kwenye maeneo yote. Hilo ndilo tutampima Katibu Mkuu Afya na TAMISEMI. Hii kero tunaimudu kuitatua, hatupaswi kuona upungufu wa vitabu vya kliniki nchini,” alisema.