Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dkt. Said Mohamed, ametangaza kuwa kuanzia mwaka huu hakutakuwa na maswali ya kuchagua katika mitihani ya Hisabati.
Hatua hii inalenga kuboresha uelewa na umahiri wa wanafunzi katika somo hilo muhimu. Dkt. Mohamed alitoa taarifa hii wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi katika hafla iliyofanyika Jijini Tanga.
Katika taarifa yake, Dkt. Mohamed alieleza kuwa tayari mafunzo yameshatolewa kwa walimu ili kutekeleza mabadiliko haya. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu katika kuhakikisha mpango huu unafanikiwa.
“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ililiagiza Baraza kufanya tathmini ya hali ya ufaulu na ujifunzaji wa wanafunzi katika masomo ya Hisabati, Bailojia, Fizikia na Lugha ya Kiingereza,” alisema Dkt. Mohamed. Aliongeza kuwa lengo la tathmini hii ni kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika masomo hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, aliyekuwepo katika hafla hiyo, alibainisha kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati ya kupima ubora wa elimu kitaifa na kimataifa. Prof. Mkenda alisema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuboresha ubora wa elimu nchini na kwamba ni muhimu kujipima ili kuona elimu yetu ipo katika hali gani ikilinganishwa na viwango vya kimataifa.
“Mageuzi ya elimu yaliyofanyika yana maana pana na yameleta mfumo tofauti wa elimu nchini. Ni muhimu kuwa na tathmini ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora,” alisema Prof. Mkenda. Aliongeza kuwa suala la kuwa na tathmini ya kweli ni muhimu kwa kuwa linahakikisha mfumo wa mtihani una weledi na uadilifu, hali itakayosaidia kupata matokeo yenye uhakika.
SomaZaidi;Mitihani ya Kidato cha Sita na Ualimu Yashika Kasi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, alieleza kuwa ayari mafunzo yameshatolewa kwa walimu ili kutekeleza mabadiliko haya. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu katika kuhakikisha mpango huu unafanikiwa.
Prof. Nombo aliongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kushirikiana na wadau wa elimu katika kuhakikisha masuala ya ufundishaji, ujifunzaji na tathmini katika shule yanaimarishwa kwa lengo la kukuza umahiri wa wanafunzi katika masomo. Alisisitiza kuwa hatua hizi ni muhimu katika kujenga msingi imara wa elimu kwa watoto wa Tanzania.
Kwa muktadha huo, mabadiliko haya yanaashiria juhudi kubwa zinazofanywa na serikali na wadau wa elimu nchini katika kuboresha ubora wa elimu. Wanafunzi sasa wanapaswa kujitayarisha kwa mabadiliko haya mapya katika mitihani ya Hisabati, huku walimu wakitarajiwa kutumia mbinu bora zaidi za ufundishaji ili kuhakikisha wanafunzi wanaelewa vizuri zaidi na siyo kuhifadhi majibu tu.
Hatua ya kuondoa maswali ya kuchagua inachukuliwa kama sehemu ya mikakati ya kuinua kiwango cha uelewa na umahiri wa wanafunzi katika masomo ya sayansi na hisabati, masomo ambayo ni msingi muhimu katika maendeleo ya teknolojia na uvumbuzi. Hii ni fursa kwa walimu na wanafunzi kujikita zaidi katika ufahamu wa kina wa mada zinazofundishwa na kujiandaa kwa changamoto mpya zinazokuja na mfumo huu mpya wa tathmini.