Wataalam wa afya nchini wamewatoa hofu wananchi usalama wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka tisa hadi 14.
Tangu kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo, kumekuwa na hofu kwa jamii hasa wazazi kuhusu usalama, huku baadhi wakiwazuia watoto wao kuchanja wakiamini zimeletwa kupunguza uwezo wa Watanzania kuzaa.
Soma Zaidi;Afya ya Akili Inavyo Watesa Watu
Maswali ni kuhusu umri wa watoto wanaopatiwa chanjo hiyo wa chini ya miaka 14 ilhali madhara huonekana kuanzia miaka 24.
Aidha, watoto wa kiume kutopatiwa chanjo hiyo na dozi kuwa moja badala ya tatu kama awali, huku wanaoshi na VVU kupata dozi tatu tofauti na wengine.
Vile vile, muda wa chanjo kuimarisha kinga ya mtumiaji na kama ni hiyari na madhara kwa asiyepatiwa chanjo hiyo.
Jopo la madaktari na watafiti wabobezi katika afya ya uzazi walifanya mjadala ulioendeshwa na jukwaa la Jamii Forum kupitia mtandao wa kijamii wa X, na kueleza kuwa kuna umuhimu wa chanjo hiyo kwa kundi lengwa la watoto.
Akizungumzia usalama wa chanjo hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, amewatoa hofu Watanzania kuwa tangu ianze kutolewa mwaka 2014 kwa wakazi wa Kilimanjaro hawajapata taarifa ya mtumiaji kupata madhara yoyote.
Amesema utoaji wa chanjo hizo katika awamu ya kwanza ulienda sambamba na ufuatiliaji wa karibu, ili kuchunguza kama kuna madhara yoyote makubwa yanayoweza kujitokeza na kuyafanyia kazi, lakini hakukuwa na taarifa yoyote.
Amesema baada ya kujiridhisha na usalama wake waliendelea kutoa chanjo hiyo na mwaka 2018 waliizindua rasmi, na kuendelea kuitoa kwa dozi ya mara mbili kila baada ya miezi sita, lakini mwaka huu wamebadili na kutoa moja baada ya utafiti kuonyesha zote zinafanya kazi sawa.
Amesema serikali imetilia mkazo kutolewa kwa chanjo hiyo kwa sababu saratani ya mlango wa kizazi ndio inayoongoza kuathiri watu kwa asilimia 23 kati ya aina zote za saratani zilizopo nchini, ikifuatiwa na saratani ya mfumo wa chakula na matiti.
“Gharama ya matibabu ya saratani hususani ya mlango wa kizazi, serikali imefanya uchambuzi na kuona kwamba mtu anayekwenda kwa matibabu ya saratani hiyo ina mgharimu zaidi ya Shilingi milioni nane kwa kuanzia na zaidi kutegemea na ukubwa wa ugonjwa,” amesema.
Akijibu swali la mshiriki aliyetaka kufahamu kama chanjo hiyo ina uwezo wa kuzuia mwanamke kubeba ujauzito, Daktari Mkufunzi kutoka Wizara ya Afya, Norman Jonas, amesema kuwa hakuna uhusiano wowote wa chanjo hiyo na mtu kutobeba ujauzito.
“Tafiti za kisanyansi zinaonesha umri sahihi wa kutoa chanjo ni miaka tisa hadi 14 ikiaminika ni umri ambao ni kabla ya balehe. Virusi vya HPV vinaathiri binadamu, na maambukizi yake yanapotokea hayana dalili,” amesema.
Amesema virusi vya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) vinaathiri watu wengi na havina dalili, kati ya watu 100 waliopata maambukizi ya ugonjwa huo, 90 yawametokana na virusi hivyo vilivyopo vya aina 200, huku asilimia 40 ya maambukizi yakipatikana kupitia kushiriki ngono.
Akijibu swali la mdau aliyetaka kufahamu kwa nini chanjo hiyo inatolewa kwa mabinti wa umri wa miaka tisa hadi 14 ilhali watu walio hatarini kupata maambukizi ni kuanzia miaka 25, Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dk. Florian Tinuga, amesema hutolewa kwa watoto wa umri huo kwa kuzingatia utafiti wa kisayansi.
Amesema chanjo hiyo ni hiyari, lakini anashauri watoto wapatiwe kwa sababu ni muhimu na salama kwa mabinti hao, na inatolewa bure katika vituo vya afya na hospitali za serikali na binafsi pamoja na kuwafuata watoto hao katika shule wanazosoma.
Amesema katika kundi hilo chanjo ya dozi tatu itatolewa kwa mabinti wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wasioishi na virusi hivyo watapatiwa dozi moja.
Amesema hadi kufikia Aprili 26, mwaka huu ugawaji wa chanjo ya dozi moja ya HPV uliwafikia karibu asilimia 90 ya walengwa tangu kuanza kutolewa Aprili 22, mwaka huu hali inayoonyesha kuna hamasa kubwa katika jamii.
WENYE VVU
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mataalam wa Magonjwa ya Jamii, Dk. Maryam Amour, amewashauri wenye VVU kufanya uchunguzi wa saratani hiyo wakiwa na umri wa kuanzia miaka 25 kwa kuwa wapo hatarini zaidi kupata maambukizi.
Ametaja kundi lingine lililo hatarini ni wanawake walio katika umri wa miaka 30 hadi 50 na kuwashauri kufanya uchunguzi kila baada ya miaka mitatu, ili wanapobainika waanze tiba mapema kabla ugonjwa haujawa mkubwa na kushindwa kutibika.
Amesema utatifi uliofanyika katika nchi tisa ikiwamo Tanzania ulionesha wasichana wengi wanaanza kujamiiana wakifikisha umri wa miaka 15 na kuendelea, ndio maana hata chanjo hiyo imeanza kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 14 ili kuwaepusha kupata maambukizi wakiwa na umri mdogo.
Dk. Maryam amesema nchi zilizoanza kutoa chanjo hizo kwa muda mrefu na kuchanja zaidi ya asilimia 90 ya walengwa ikiwamo Australia wamefanikiwa kupunguza matukio yote yanayotokana na maambukizi ya kirusi cha HVP.
“Australia pamoja nchi nyingine 40 zinatoa dozi moja ya chanjo hiyo kama ilivyo Tanzania na ukiangalia kwenye takwimu Australia ndio nchi yenye kesi chache za kansa ya mlango wa kizazi ulimwenguni na kufikia malengo ya dunia,” amesema.
Amesema Tanzania kwa sasa wanachanja watoto wa kike pekee kutokana na uwezo, lakini tatizo hilo linawapata na wanaume.
WAZAZI WANENA
Mmoja wa wazazi walioshiriki mjadala huo, Happy Enea, amesema amejifunza na kupata uelewa mpana kuhusu chanjo hiyo kupitia kwa madaktari hao na atamruhusu mtoto wake apatiwe chanjo hiyo shuleni au kumpeleka kwenye kituo.
Kabla ya kupata elimu hiyo alimkataza mwanawe kupata chanjo hiyo akiamini itamletea madhara ikiwamo kutobeba ujauzito kutokana na maneno aliyokuwa akiyasikia kwa watu.
“Akiwa shule ya msingi walimu walinipigia simu mara mbili kunishauri mwanangu apatiwe hiyo chanjo nikakataa, juzi pia akiwa sekondari walimu wake walinipigia simu nikakataa, lakini jana nikasema kwa nini nisiingie kwenye huu mjadala nisikie mwenyewe kama kweli kuna madhara, kumbe hakuna ni salama,” amesema Happy.
Aidha, ameishauri serikali kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa jamii ikiwezekana elimu hiyo itolewe hospitali kwa wagonjwa wanaokwenda kila siku, vituo vya mabasi, ofisini na hata kuweka matangazo kwenye luninga ili elimu iwafikie watu wengi zaidi kwa kuwa sio kila mtu ana uwezo wa kusikiliza mijadala ya mitandaoni.