BAADA ya miaka 60 ya uhusiano wa kihistoria, Tanzania na China zimetangaza kuingia katika zama mpya za uhusiano wa kidiplomasia, zenye lengo la kujenga dunia bora zaidi yenye maendeleo na usalama.
Soma zaidi;China and Tanzania Mark 60 Years of Strong Collaboration
Katika mkutano uliofanyika jijini Beijing, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, alimweleza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, kuhusu umuhimu wa uhusiano huo wa muda mrefu. “Tanzania mara zote imekuwa rafiki wa kweli wa China. Miaka 60 ina maana kubwa sana kwetu.
Hatua inayofuata sasa ni kuendeleza uhusiano huu katika zama mpya za kujenga dunia yenye maendeleo, haki, na usalama kwa watu wote,” alisema Wang. Makamba, ambaye yuko nchini China kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Wang, alieleza namna Tanzania inavyothamini mchango wa China katika maendeleo yake na kwamba wakati umefika wa kuingia katika zama mpya zitakazozingatia changamoto za dunia ya sasa.
“China ni rafiki zetu wa kweli. Baada ya miaka hii 60, sasa tuingie katika zama mpya za uhusiano zinazozingatia changamoto zilizopo kwenye kujenga dunia bora zaidi,” alisema. Katika kuonyesha uhusiano wa karibu baina ya wananchi wa mataifa hayo, Wang alisema China inatoa dola 500,000 za Marekani (sawa na shilingi bilioni 1.3) kusaidia waathirika wa mafuriko ya mvua nchini Tanzania. Maeneo kadhaa ya Tanzania yameathiriwa na mvua kubwa za masika na El Nino, na mchango huo umetolewa ili kusaidia waathirika kuanza upya maisha yao.
Makamba alishukuru kwa mchango huo akisema ni ushahidi wa urafiki wa kipekee baina ya nchi hizo mbili. Katika hatua nyingine, Serikali ya China imetoa mwaliko rasmi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria mkutano wa masuala ya usalama baina ya China na Afrika (FOCAC) uliopangwa kufanyika Septemba mwaka huu. Mkutano wa FOCAC hufanyika kila baada ya miaka mitatu na ni miongoni mwa mikutano muhimu kwenye uhusiano wa kimkakati baina ya nchi za Afrika na China.
Pia, China imekubali ombi la Tanzania la kufanya maboresho ya Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Salim Ahmed Salim, ikiwemo kuongeza majengo, mitaala na kukifanya kuwa cha kimkakati kwa masuala ya kidiplomasia. Dk. Salim ni mmoja wa wanadiplomasia wa Tanzania wenye heshima kubwa nchini China, na uamuzi wa kuongeza hadhi ya chuo hicho umezingatia umuhimu wake kwa nchi hizo mbili. Katika ziara yake hiyo inayoendelea nchini China, Makamba, aliambatana na Mbunge Zahor Haji, alitembelea na kufanya mazungumzo na taasisi na viongozi wa mashirika yanayohusika na misaada kwa Tanzania, ikiwemo benki ya EXIM ambayo imeahidi kuendelea kukopesha miradi ya kimkakati.