Mhe. Jerry Silaa, amefanya hatua muhimu katika kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi katika Jiji la Dodoma. Katika ziara yake, Mhe. Silaa ameifunga rasmi Ofisi za Masijala ya Ardhi katika jiji hilo, akiwa na lengo la kuondoa changamoto zinazokabili wananchi katika kupata huduma bora za ardhi.
Katika hotuba yake, Mhe. Silaa ameeleza kuwa, “Tumeamua kufunga masijala hii ya jiji, nimetoka kuweka makufuli tumeifunga. Tunahamisha shughuli hizi za ardhi kutoka hapa kuja ofisini kwangu kwa Waziri wa Ardhi.” Aidha, ameeleza kuwa, sababu ya kufunga ofisi hizo ni kuondoa matatizo ya wananchi ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata huduma za ardhi.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza kuhakikisha kuwa haki za wananchi zinasimamiwa ipasavyo. “Dkt. Samia ametuelekeza tusimamie haki za watu wake, na kazi hiyo tutaifanya kwa uadilifu mkubwa na ukisoma vitabu vyote vinavyoelezea kazi ya haki ni kazi ya kimungu,” amesisitiza Mhe. Silaa.
Aidha, Mhe. Silaa amewaambia wananchi kuwa, ofisi za ardhi zitafunguliwa rasmi tarehe 3 Juni 2024 katika jengo lililokuwa la Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Katika ofisi hizo, Waziri ameahidi kujenga mazingira bora ya huduma, ikiwemo kuweka kamera zenye uwezo wa kuchukua sauti na picha, ambazo atakuwa na uwezo wa kuzifuatilia hata akiwa mbali.
ReadMore;Matumizi Ya Ardhi Yazingatiwe Yasibadilishwe Bila Kibali- Silaa
“Naenda kujenga ofisi ya kisasa itakuwa na jicho langu mimi moja kwa moja tutaweka maafisa waadilifu binadamu wa siku hizi siyo binadamu wa zamani tutaweka kamera zitachukua picha na sauti na wakati nikiwa Dar es Salaam na jimboni katika ziara nina uwezo wa kuingia kwenye simu yangu kuangalia ofisi za ardhi dodoma wanafanya nini,” amesema Mhe. Silaa.
Kwa mujibu wa Waziri, lengo la mabadiliko haya ni kuwezesha wananchi kupata huduma bora za ardhi kwa wakati unaofaa na bila kuweka vikwazo vya vyumba vya kufungiwa. Aidha, ameahidi kuwa, Wizara itaweka maafisa waadilifu watakaohakikisha kuwa haki za wananchi zinatunzwa ipasavyo.
Hatua hii ya Waziri Silaa inaonyesha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi nchini, huku ikilenga kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma bora na kwa wakati unaofaa.