Saa moja lilitosha jana kuafikiana na kutamatisha rufani namba 155 ya Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 27 iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai,mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, na wenzake sita katika Mahakama Kuu ya Tanzania , Kanda ya Arusha.
Mazungumzo hayo yalikuwa kati ya mawakili wa serikali na wale wanaomtetea Sabaya.
Soma ZaidiMbowe: Tathmini Ya Maandamano Kwa Mikoa 13
Baada ya majadiliano hayo ya pande mbili, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliiandikia mahakama hiyo barua rasmi ya kutokuwa na nia ya kuendelea na rufani kisha kuiondoa mahakamani.
Katika rufani hiyo, mleta rufani alikuwa DPP na wajibu rufani ni Ole Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), John Odemba, Jackson Macha(29) na Nathan Msuya (31).
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama, Wakili wa Sabaya, Mosses Mahuna, alisema rufani ilikwenda kwa ajili ya kusikilizwa kabla ya wao kupeleka maombi Mahakama ya Rufani kuomba ifanye mapitio na marejeo ya mwenendo wa usikilizaji wa kesi hiyo kwa kuwa hawakuridhika nao.
“Baada ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufanya marejeo na mapitio ya namna shauri lilivyokuwa likiendeshwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliamua kufuta mwenendo mzima na kuamua rufani hii kuanza kuendelea kusikilizawa upya.
“Leo (jana) rufani hii imeitwa kwa ajili ya kusikilizwa baada ya uamuzi ule wa Mahakama ya Rufani wa kubatilisha mwenendo ambao ulikuwa umeanza kusikiliza awali,” alieleza Mahuna.
Wakili Mahuna alisema baada ya kufika mahakamani kwa lengo la kusikilizwa kwa rufani DPP, aliwasilisha notisi ya kuifahamisha mahakama kuwa, hana nia ya kuendelea na rufani hiyo.
“Mahakama baada ya kupokea notisi ya DPP, imefuta rufani hii rasmi leo (jana) mbele ya mahakama, hivyo Sabaya hana tena kesi inayomkabili kwa kuwa, zote zimekwisha malizika,”alieleza Mahuna.
Juni 4, 2021, Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka matano yaliyokuwa yakiwakabili katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27.
Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza lilikuwa kuongoza genge la uhalifu kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Kifungu cha 57(1) na 60(2).
Shtaka la pili lilikuwa la kujihusisha na vitendo vya rushwa na lilikuwa linamkabili Sabaya pekee na ilidaiwa ni kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kifungu cha 15(1B,2) Sura ya 329, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Shtaka la tatu lilikuwa la kujihusisha na vitendo vya rushwa na lilikuwa likimkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake ambalo lilidaiwa kuwa kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kifungu cha 15(1B,2) Sura ya 329, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Shtaka la nne lilikuwa la matumizi mabaya ya Madaraka. Shtaka hilo lilikuwa likimkabili Sabaya peke yake huku ikidaiwa kuwa ni kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Shtaka la tano ni utakatishaji wa fedha na lilikuwa likiwakabili washtakiwa wote na ilidaiwa mahakamani ni kinyume na kifungu 12(D),13(1A), cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 423, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.