Sakata la pambano la Bondia Hassan Mwakinyo na Patrick Allotey kutoka Ghana limemalizika rasmi baada ya wawili hao kuzichapa usiku wa kuamkia leo.
Mwakinyo ameshinda pambano hilo lilofanyika Dar es salaam kwa TKO baada ya Allotey kushindwa kuendelea na pambano raundi ya pili ilipomalizika akieleza kuwa ameumia bega na ndipo ‘Champez’ alipotangazwa mshindi.
Hata hivyo katika raundi hizo mbili Mwakinyo alionesha uchu wa kutaka ushindi akirusha makonde mazito kwa mpinzani wake.
Ushindi huo unamfanya bondia huyo kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBO.
Soma Zaidi:Mwakinyo yuko tayari kupambana na mpinzani wake
Pambano hilo lilipaswa kupigwa usiku wa Mei 31, 2024 lakini ilishindikana kutokana na Mwakilishi kutoka WBO kutolipwa fedha zake kitendo ambacho Mwakinyo amenukuliwa akisema tunautia doa mchezo wa ngumi huku akitupa lawama kwa promota wa pambano hilo.
Mwakinyo ameandika yafuatayo “Guys naomba niombe radhi Mashabiki wangu wote na niweke wazi kwenu kitu kimoja kulingana na sitofahamu iliyotokea juzi kwa mimi kutocheza kwenye pambano langu lililotarajiwa na wengi wenu, NAOMBA NIANDIKE KWA HERUFI KUBWA YA KWAMBA AZAM TV HAWANA CHUKI WALA BIFU YOYOTE NA MIMI kama inavyo tafsiriwa na wengi”
“Binafsi kilichotokea juzi wamejitahidi sana kupambana kisitokee nimeona jitihada zao kubwa sana zikifanyika kunusuru lile pambano kuanzia ngazi za juu mpaka chini ya uwongozi, yani hata kulipokuwa na taarifa ya pambano kufutwa na Uongozi wa chama cha ngumi ilikuwa ni sawa kabisa, walishaona kuna mapungufu mengi ambayo walijua yangetokea haya, anyway kiufupi ipo haja sasa ya sisi Wapiganaji kupewa fursa na kipaumbele cha kufanya kazi kupitia promoshen zetu”
“Hii itasaidia kuepeusha matatizo ya lazima yanayoweza kujitokeza kwa Mapromota Wahuni waongo kama ilivyotokea, na ni vile sasa nimekua nafikiri zaidi kabla ya kufanya kitu lakini kama nisingefanikiwa kupigana lile pambano jana kwa jitihada zangu binafsi basi huwenda sasa ningekuwa Osterbay Police kwa jinai mbaya kubwa ambayo pengine ingepumbazisha fikra na akili ya kila ambaye angeskia, all in all nawashukuru sana Mashabiki zangu ambao hawakusita kufika na kuungana na mimi na wote ambao wamekua wakifuatilia wakati wote Mwenyezi Mungu atawalipa zaidi ya mapenzi yenu”
Kanuni zinaeleza kuwa Mwakinyo asingecheza mchezo huo angepokonywa mkanda huo hivyo bondia huyo alilazimika kuchipa usiku wa jana baada ya vikao vingi vya kujadili hatma ya pambano hilo kufanyika.